Wanamgambo wamewapiga risasi na kuwauwa wafanyakazi wanne wa serikali katikati mwa Kabul katika makabiliano ya hivi karibuni kuwahi kutokea katika mji mkuu huo wa Afghanistan.
Msemaji wa jeshi la polisi mjini Kabul Ferdaws Faramarz amewaambia waandishi habari kwamba watu waliokuwa na bunduki walifyetua risasi dhidi ya gari lililokuwa limewabeba wafanyakazi wa wizara ya shughuli ya ukarabati wa maeneo ya vijijini na maendeleo na kuwauwa wafanyakazi wanne.
Aidha shambulio jingine limefanyika pia ambapo mtu mmoja alijeruhiwa baada ya bomu lililolengwa kuripuliwa dhidi ya gari la serikali. Kwa ujumla mashambulizi hayo ya leo yamefanywa siku moja baada ya kutokea mashambulizi mengine matatu ya mabomu katika mji mkuu huo wa Afghanistan.
Kuongezeka kwa mashambulizi kunatokea wakati mazungumzo ya amani kati ya Taliban na serikali yaliyoanza mwezi Septemba mwaka jana kukwama.