Ugonjwa wa kisukari unahatarisha zaidi maisha ya wagonjwa wanaopata maambukizi na kulazwa hospitalini kutokana na virusi vya corona (Covid-19).
Kulingana na shirika la habari la UPI lenye makao yake makuu nchini Marekani, data za wagonjwa 2,800 wanaougua kisukari ambao walipata matibabu ya virusi katika hospitali 68 tofauti nchini Ufaransa, zilitathminiwa katika upeo wa utafiti uliofanywa na wataalam wa ugonjwa wa kisukari wa Chuo Kikuu cha Nantes nchini Ufaransa .
Matokeo yaliyopatikana yalionyesha kuwa mmoja kati ya wagonjwa 5 wa kisukari waliolazwa hospitali kwa matibabu ya Covid-19, walifariki ndani ya mwezi mmoja.
Kwa kuongezea, ilibainishwa kuwa hatari ya kifo kutokana na Covid-19 kwa wagonjwa walio na kisukari kwa kiwango cha hali ya juu ambao hutumia insulini ya kawaida, ilikuwa asilimia 44 zaidi kuliko wagonjwa wa kisukari ambao hawatumii insulini.
Wataalam walisisitiza kuwa udhibiti wa kiwango cha sukari ya damu kwa wagonjwa walio na kisukari kwa kutumia matibabu ya kawaida kuna umuhimu mkubwa katika kuzuia vifo vinavyosababishwa na Covid-19
Watafiti pia wameweka msisitizo kwamba wagonjwa wa kisukari wako katika kundi hatari zaidi na wanapaswa kupewa kipaumbele katika suala la chanjo.