HALMASHAURI ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imetoa motisha ya vitu mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi, mabegi kwa wanafunzi na vyeti kwa walimu wa shule za msingi zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa mwaka jana.
Katika hafla iliyofanyika katika Mji Mdogo wa Kibara wilayani Bunda, Ofisa Elimu (Msingi) wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Reginald Richard, alisema mwaka jana halmashauri hiyo ilifanya vizuri na kuwa ya tatu kimkoa katika matokeo ya darasa la saba hivyo, vitu vilivyotolewa vinalenga kuwatia moyo walimu na wanafunzi wa shule hizo ili waendelee kufanya vizuri.
Alisema kutokana na shule hizo kufanya vizuri, wameamua kutoa motisha hiyo ya vifaa mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi kwa walimu pamoja na kuwapatia vyeti kama ishara yakutambua mchango wao huku wanafunzi wakipewa motisha ya mabegi.
Hata hivyo alisema, licha ya kuwapo mafanikio hayo kitaaluma, zipo changamoto kadhaa zinazoikabili idara ya elimu.
“Zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili idara yetu ya elimu, ukiwemo utoro kwa baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi, lakini hili tunalifanyia kazi ili kulikomesha,” alisema Richard.
Akitoa motisha kwa shule hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Amosi Kusaja, alizipongeza shule zote zilizofanya vizuri na kusema idara ya elimu inaongoza kwa vitendo katika halmashauri hiyo.
Aliitaka halmashauri hiyo kuendelea kutekeleza wajibu wake ipasavyo ili kuinua kiwango cha taaluma kwa shule zote zilizoko katika halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, alisema walimu ndio nguzo muhimu katika kuandaa wataalamu mbalimbali pamoja na viongozi, lakini wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali na alizotaka wakabili bila kukata tamaa.
Wakipokea motisha hiyo kwa niaba ya shule zilizofanya vizuri, walimu Malindi Majige na Magdalena Mtei, waliahidi kuendelea kufanya vizuri kitaaluma kwani hali hiyo inawatia moyo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Fredence Serapion, aliwataka walimu kuongeza bidii ili kuongeza ufaulu zaidi kwenye shule zao ili hatimaye Mkoa wa Mara uwe katika kumi bora kitaifa.