Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku 14 kwa wadaiwa (defaulters) wa makusanyo ya mapato ya Halmashauri wakiwemo watendaji wa vijiji na Kata kuhakikisha wanarudisha fedha hizo kabla ya Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo kuwafikisha mahakamani wadaiwa hao.
Mh. Wangabo amesisitiza kuwa pamoja na hatua kadhaa alizowahi kuchukua hapo nyuma kwa kuwakabidhi wadaiwa hao kwa TAKUKURU lakini bado hali imeendelea kubaki kama ilivyokuwa na huku halmashauri zikiendelea kulalamika kuwa na mapato finyu ilhali kuna wanaokusanya mapato ya serikali ya kutumia watakavyo.
Aidha, Ameongeza kuwa pamoja na hali hiyo hakuna hata Mkurugenzi mmoja wa Halmashauri kati ya halmashauri nne za mkoa huo aliyewahi kuwachukulia hatua wadaiwa hao ama hata kuonyesha kuguswa na ubadhirifu huo matokeo yake malalamiko yanatolewa na mtu ambaye yupo nje ya halmashauri.
“Sasa hawa wote ambao wame-default hizi milioni 932, ninawapa wiki mbili tu wawe wamezirudisha hizi fedha, vinginevyo TAKUKURU peleka mahakamani hawa watu, wala sio tena ule mchezo wa kubembelezana kwamba leta kesho leta keshokutwa, wapelekwe na nipate taarifa ya kupelekwa mahakamani mwezi ujao, ninatoa wiki mbili wawe wamerudisha hizi fedha zote, haw ani wezi na hatuwezi kuwavumilia,” Alisisitiza.
“Halafu unakuta mtu ame-default mwaka jana, huyo huyo ndio bado yupo pale pale, sijui hicho kituo ndio kinakusanya mapato mengi, huyo huyo anapewa tena kukusanya hapo mahali, hatuwezi kwenda namna hii, halmashauri zetu tunazi-paralise, tunazimaliza, tunazifilisi, mchwa hawa lazima tuwashughulikie, vinginevyo watakuwa wanaendelea kila siku katika hali hiyo hiyo, wanaona ni mchezo wa paukwa pakawa,” Alisema.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilifanyika tarehe 23.2.2020 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na kuhudhuriwa na wajumbe wakiwemo wabunge wa Mkoa huo, Wenyeviti wa halmashauri, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na kuongozwa na Mkuu wa mkoa.
Kwa mwaka huu wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri za mkoa wa Rukwa zilikisia kukusanya Shilingi 9,487,289,000 hata hivyo katika nusu ya Kwanza ya mwaka huo wa fedha kuanzia Julai hadi Disemba, 2020 halamshauri hizo zimekusanya kiasi cha shilingi 3,682,531,918.16 sawa na asilimia 38.8 amabpo zilipaswa kukusanya angalau asilimia 50.