WASTARA Juma Kilowoko ni mmoja wa mastaa wa fi lamu hapa nchini waliopitia changamoto nyingi katika maisha yake tangu utotoni mpaka sasa.
Miaka kadhaa iliyopita alipoteza mguu wake, akampoteza mume wake mpenzi ambaye pia alikuwa ni msanii wa filamu, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ lakini bado maradhi yaliamuandama kwa kiasi kikubwa kila kukicha.
Akipiga stori na AMANI, Wastara anasema japokuwa amekutana na changamoto nyingi lakini hakukata tamaa kwenye maisha yake kwani anasema kuwa moyo wake umeshaota sugu nyingi hivyo chochote mbele yake anakikabili na maisha yanaendelea.
Msanii huyu alizungumza mambo mengi yanaondelea kwake hivi sasa, fuatilia mahojiano haya kwa kina.
AMANI: Habari za siku Wastara? kuna kipindi ulipotea kabisa!
WASTARA: Nipo, kwa sababu maisha ya sasa hivi hayatabiriki hata kidogo ndio maana nimekuwa kimya sana.
AMANI: Naona kama umepoa kwenye filamu hivi?
WASTARA: Sijapoa, lakini sasa hivi unaona mambo mengi ni kwenye tamthilia na hivyo hapa Bongo, hakuna ambaye hajui uwezo wangu hata kidogo, lakini basi unawaacha tu waendelee na mimi niko mbioni kuitengeneza yangu.
AMANI: Lakini ulikuwa hodari sana wa kutengeneza fi lamu zako nyingi mwenyewe, sijui sasa hivi nini kimetokea?
WASTARA: Ni kweli lakini mambo yanaenda yanabadilika majukumu
WASTARA: ni mengi lakini hakuna neno nitasimama tena kama zamani.
AMANI: Niliona uliandika kwenye mtandao wako wa kijamii ukizungumzia kuhusu kuumizwa kimapenzi nini kimekupata tena?
WASTARA: Katika maisha yangu hapa duniani nimewahi kupendwa na mtu mmoja mtu ambaye ameshatangulia mbele ya haki, ni mume wangu Sajuki, wengine wanakuja kwako kwa maslahi tu na si vinginevyo, mwingine anakuchapa kutokana na ulemavu wako ambao unao.
AMANI: Kwanini unasema anatumia ulemavu wako kama fimbo?
WASTARA: Mwingine anaona kama hilo ndilo udhaifu wako wa kukuumiza kwa kila unalofanya, kumbe Mungu ndio anajua kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu yeye anaweza akajiona mzima kumbe sekunde tu anaweza kuwa hata zaidi ya mimi.
AMANI: Hivi karibuni niliona unafanya mnada ulikuwa ni wa nini
WASTARA: Nilikuwa nauza sabuni zangu na mafuta ili nitakachokipata niweze kuwasaidia yatima wezangu kama mimi.
AMANI: Kwanini uliamua kugawa nguo zako?
WASTARA: Nimeamua hivyo kwa sababu kuna watu wengine wanauhitaji hawana mavazi na hawana hata cha kujifunika na mimi nikaona ninazo nyingi ndani kwanini nisiwagawie wezangu na ninajua wazi uchungu wa kuishi kwenye maisha duni au kupoteza wazazi.
AMANI: Kuna kipindi ulikuwa ukiimba, vipi iliishia wapi na kipaji hicho?
WASTARA: Mimi bado naimba sana, sema tu bado sijajipanga zaidi kwa kujikita kwenye mambo ya muziki, lakini niko vizuri sana na nina nyimbo zangu nyingi ipo siku nitaziachia hivi karibuni.
AMANI: Vipi kuhusu mtoto wako uliozaa na Sajuki?
WASTARA: Yupo na anaendelea vizuri sana, na nina farijika sana kila ninapomuona kwa sababu kafanana na baba yake mno.
AMANI: Mimi naomba nikushukuru sana Wastara kwa ushirikiano wako.
WASTARA: Asante sana Mungu akubariki.
MAKALA: IMELDA MTEMA WETU NA MITANDAO