WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekabidhi magari mawili kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi yatakayowezesha askari kutoa huduma katika maeneo ya mkoa huo.
Amekabidhi magari hayo jana (Jumatatu, Februari 21, 2021) baada ya kuzungumza na wananchi katika kituo cha Polisi Mtama ambako makabidhiano hayo yalifanyika.
Magari yaliyokabidhiwa ni Toyota Land Cruiser Pickup yenye namba za usajili PT 2615 na Toyota Land Cruiser V6 lenye namba za usajili PT 4378.
Kati ya magari hayo gari moja TP 4378 ni kwa ajili ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi na gari lingine PT 2615 ni kwa ajili ya kituo cha polisi cha Mtama.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kutoa vitendea kazi kwa jeshi la polisi kadiri inavyowezekana ili kuwawezesha askari nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
`Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi Mtatiro Kitinkwi alisema magari hayo yatawezesha shughuli za doria kufanyika kwa uhakika.
”Magari haya unayotukabidhi leo (jana) yatawezesha shughuli za usafiri wa polisi, doria na usafirishaji wa mahabusu kufanyika kwa uhakika kulingana na jiografia ya halmashauri ya Mtama.”
Kamanda Kitinkwi aliiomba Serikali kukimalizia kituo cha Polisi cha Mtama kwa kuweka samani na kujenga kambi ya makazi ya askari katika kituo hicho.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kwa niaba ya wananchi aliishukuru Serikali kwa kutoa magari hayo ambayo yatawezesha shughuli za ulinzi na usalama katika jimbo hilo na Mkoa kufanyika kwa ufanisi zaidi.