Waziri wa Afya ajiuzulu kashfa chanjo ya corona

 


Waziri wa Afya nchini Peru, Pilar Mazzetti ametangaza kujiuzulu kutokana na kashfa kwamba Rais wa zamani wa nchi hiyo, Martin Vizcarra alidungwa kabla Serikali haijatangaza kuanza kufanya hivyo kwa raia wake.

 

Ingawa Serikali bado haijathibitisha, lakini Televisheni ya Taifa nchini humo imesema Waziri Mazzetti aliyeteuliwa Julai mwaka jana kuutumikia wadhifa huo, amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais Francisco Sagasti.

 

Mazzetti anakuwa waziri wa tano kwa nchi za Amerika Kusin kujiuzulu tangu kuibuka kwa janga la corona mwishoni mwa mwaka 2019. Virusi vya corona vilithibitika nchini Peru miezi 11 iliyopita.

 

Mpaka sasa, Taifa hilo bado linasumbuliwa na janga hilo, hasa mlipuko wa awamu ya pili kwani zaidi ya wagonjwa 14,100 wamelazwa katika hospitali zake na nyingi zikisema zimeelemewa na zinashindwa kuwahudumia wanaoshindwa kupumua.

 

Katika kukabiliana na virusi hivyo, wananchi wa Peru walianza kuchanjwa Jumanne iliyopita, siku mbili baada ya kupokea dozi 300,000 kutoka kampuni ya Sinopharm inayomilikiwa na Serikali ya China.

 

Hata hivyo, Alhamisi iliyopita, gazeti la Peru 21 liliripoti kwamba Rais Vizcarra alipata chanjo hiyo kwa siri tangu Oktoba mwaka jana, wiki chache kabla hajapinduliwa kwa tuhuma za “kutokuwa na uwezo.”

 

Rais Vizcarra mwenyewe amesisitiza kuwa alijitolewa kushiriki majaribio ya chanjo hiyo inayotengenezwa na Sinopharm.

 

“Nilikuwa miongoni mwa watu 12,000 waliojitolea kushiriki majaribio hayo,” alisema Rais huyo ambaye kwa sasa anaendelea na kampeni za uchaguzi wa wabunge utakaofanyika Aprili.


Vizcarra (57) alisema aliuficha ukweli huo na kwamba hata mkewe pia alikuwa miongoni mwa walioshiriki majaribio hayo, lakini lilikuwa sharti kwa waliojitolea wote kuitunza siri hiyo.


Kutokana na ukweli huo, mbunge wa upinzani nchini humo, Ali Mamani alisema chama chake kitafungua kesi dhidi ya Rais Vizcarra.


Rais Mazzetti aliyeteuliwa na Rais Vizcarra alisema hakuwa anajua chochote kuhusu siri ya mkuu wake huyo wa zamani na akakumbusha kwamba viongozi wote walio katika nafasi za uamuzi hawatakiwi kushiriki majaribio ya chanjo ili wasipindishe matokeo.




Peru yenye watu milioni 33, tayari imethibitisha zaidi ya maambukizo milioni 1.2 na vifo 43,000. Wiki hii imeanza kutoa chanjo kwa watumishi wa afya. Mamlaka bado hazijaweka wazi lini uchanjaji wa wananchi wengine utaanza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad