Shirika la Afya Dunia (WHO) limeonya dhidi ya maamuzi ya haraka kuhusu ufanisi wa chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona.
Hii ni baada ya utafiti uliofanywa Afrika Kusini kuonesha kuwa chanjo ya AstraZeneca haitakuwa na ufanisi mkubwa dhidi ya virusi vipya vya corona vilivyokumba nchi hiyo.
Lakini wataalamu wana matumaini kuwa chanjo hiyo bado itakuwa na ufanisi katika kuzuia maambukizi makali.
Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa data iliyotumiwa kwenye utafiti huo, ilikuwa ni “majaribio ya watu kidogo tu” na walioshirikishwa walikuwa “vijana wenye afya zao”.
“Ni muhimu kubaini ikiwa chanjo hiyo ina ufanisi au la katika kuzuia watu kuwa wagonjwa zaidi,” amesema katika taarifa.
Lakini pia ametambua kuwa watengenezaji wa chanjo watahitajika kuiboresha ili kukabiliana na virusi hivyo.
“Ni wazi kwamba watengenezaji wa chanjo watalazimika kuiimarisha zaidi ili kwendana na virusi vipya, hasa uzingatia virusi vya sasa kwa ajili ya siku za baadaye.
“Tunajua virusi hubadilika na tunajua tunastahili kuwa tayari kuboresha chanjo ili ziendelee kuwa na ufanisi,” amesema.