CEDRICK Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa licha ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba kupelekwa mbele wanaamini kwamba wakikutana ndani ya uwanja lazima washinde.
Awali ratiba ilikuwa inaeleza kuwa mchezo huo wa watani wa jadi ulitarajiwa kuchezwa Februari 20, Uwanja wa Mkapa ila kwa sasa utachezwa Mei 8.
Akizungumza na Spoti Xtra,Kaze alisema kuwa hawana mamlaka ya kuzungumzia kuhusu kubadilishwa kwa ratiba ya mchezo ila wanachojua wao ni kwamba lazima watakutana ndani ya uwanja.
“Kubadilishwa kwa ratiba hiyo kwetu sio tatizo, kwa kuwa mamlaka imesema iwe hivyo sisi tunajipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo ambapo kwa sasa tupo kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Mbeya City.
“Kwa kuwa tutakutana nao Mei 8 hiyo basi tunajipanga kuona kwamba tukikutana nao uwanjani tunashinda. Kwetu tunatazama mechi zote ni ngumu na ushindani ni mkubwa hivyo hatuna mashaka lazima tufanye vizuri,” alisema.
Mchezo wa raundi ya kwanza walipokutana uwanjani, Yanga ikiwa mwenyeji ngoma ilikamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Uwanja wa Mkapa.
Kwa Yanga, Michael Sarpong alimtungua Aishi Manula na kwa Simba ni Joash Onyango alimtungua Metacha Mnata.