KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa nguzo imara na muhimu katika chama hicho na pia katika siasa na demokrasia ya Tanzania.
Amesema hayo wakati akizungumza na wanahabari ikiwa ni muda mfupi baada ya Maalim Seif ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili asubuhi ya leo, Jumatano, Februari 17, 2021.
“Maalimseif alitulea kiuongozi kwa namna ambayo tutaweza kuendeleza maono yake, fikra zake na nia yake ya kuiona Tanzania yenye demokrasia na Zanzibar ambayo Wazanzibar wanaishi kwa maridhiano.
“Taarifa za maziko tutazitoa baada ya mashauriano ya karibu kati yetu kama chama na serikali kwa sababu Maalim Seif alikuwa kiongozi wa kitaifa, kwa hiyo masuala ya mazishi yake yanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na sisi chama tutaoa ushirikiano wote kwa serikali ili kuhakikisha tunamsitiri mzee wetu kwa heshima inayostahili.
“Nachukua fursa hii kama kiongozi wa chama kuwaomba Wazanzibar, wananchama wa ACT Wazalendo na Watanzania wote kuwa na utulivu katika kipindi hiki cha mtihani mkubwa sana kwetu, kuondokewa na mwamba wa demokrasia ya Tanzania na mtetezi wa maslahi ya Zanzibar.
“Kwa ndugu, familia na watoto wa marehemu tunatoa rambirambi za dhati na tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha mzee wetu anapata stara anayostahili,” amesema Zitto.