Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema kuwa mtu atakayepoteza Pasi yake ya kusafiria (Passport), itamlazimu kutoa taarifa polisi pamoja na kutangaza kwenye gazeti na kwamba ni lazima atoe kiasi cha shilingi Laki Tano kwa kupoteza Passport hiyo, na ili aweze kupata nyingine.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 16, 2021, na Msemaji Mkuu wa Idara hiyo Paul Mselle, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, saa 12:00 Asubuhi hadi saa 4:00 Asubuhi, na kuongeza kuwa uwepo wa ulazima wa faini hiyo umesaidia hata kesi za watu kupoteza passport zao kupungua.
"Passport siyo kwamba ni kitambulisho mtu anatakiwa awe nacho akaweke ndani, kwa sababu passport ukiipoteza gharama yake ni kubwa sana ili kuipata nyingine, sasa hivi kuipata hii ya kawaida ni 150,000, lakini ukipoteza utalazimika kulipa Laki Tano kwa kupoteza hiyo passport, wameiweka hiyo ili kuweka udhibiti na mtu aweze kuitunza," ameeleza Mselle
Aidha Mselle ameongeza kuwa, "Kumekuwa na changamoto ya kuchelewa kwa pasi ya kusafiria sababu unakuta mtu hajakamilisha vigezo vya kupata pasi ya kusafiria".