Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema wameandaa tukio la dakika kumi nyumbani kwa mke wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo viongozi wa kimila na dini watatoa sala zao.
Majaliwa ameeleza hayo alipokuwa akihutubia umati wa watu waliojitokeza katika uwanja wa CCM Kilumba Jijini Mwanza, kwa ajili ya kumuaga Hayati Dkt. Magufuli ambapo amesema watasimama eneo la Busisi, nyumbani kwa Mama Janeth Magufuli.
"Pale Busisi ni nyumbani kwa mke wa marehemu tumeandaa tukio la dakika kumi wazee wa mila na viongozi wa dini watatoa sala zao kisha tutandelea na safari na kisha tuingie nyumbani Chato leo," amesema Mhe. Majaliwa.
Awali akianza kuhutubia aliwaambia wananchi wa Mwanza kuwa mkoa huo ni sehemu ya historia kwa Hayati Dkt. Magufuli kwani aliishi, alifanyakazi na kujenga mahusiano na watu mbalimbali kwenye mikoa yote ya kanda ya ziwa.
"Mwanza ni mahali pa historia kwa kiongozi wetu ambaye ametutangulia, ameishi hapa amefanya kazi amejenga mahusiano na watu mbalimbali, nataka niwaambie kiongozi tunayemuaga hapa ameacha alama kila mahali hata vijini ndio manaa Watanzania kila mahali wanalia," amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa alieleza kuwa mwili wa kiongozi huyo utazungushwa ndani ya uwanja ili nkila mtu apate nafasi ya kuuga kutokana na idadi kubwa ya watanzania waliojitokeza kumuuaga.