Vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga, jioni ya leo tarehe 5 Machi 2021, imepoteza mchezo wake wa kwanza msimu huu kwenye ligi hiyo baada ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wa mchezo huo, klabu ya Coastal Unioni kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga.
Coastal Union ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mchezaji wake Erick Msagati dakika ya 10 ya mchezo ikiwa ni dakika 4 zilizopita winga wa Yanga, Tuisila Kisinda kukosa penalti iliyodakwa moja kwa moja na mlinda wa wagosi hayo wa kaya, Aboubakar Abbas.
Yanga ilisawazisha kupitia kwa Tuisila Kisinda aliyerekebisha makosa yake na kuwarudisha mchezioni mabingwa hao wakihistoria. Baada ya matokeo hayo ya sare yaliyodumu kwa muda mrefu mchezoni, alikuwa Mudathir Abdallah aliyeibuka shujaa kwa kufunga bao la pili dakika ya 84.
Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Yanga, Cedric Kaze amesema kipigo hiko kimetokana na ubora wa wapinzani wao Coastal Union bila kujali eneo la kuchezea kuathiri uchezaji wa mchezo huo.
Kwa upande wa kocha wa wenyeji, Juma Mgunda amesema ushindi huo wakihistoria umetokana na juhudi za wachezaji wake kuyafanyia kazi yale aliyokuwa anayaelekeza mazoezi hususani kucheza kwa nidhamu na tahadhari mbele ya washambuliaji wa Yanga.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea na rekodi mbaya kwenye dimba hilo, kwani tokea mwaka 2015 Yanga hawajawahi kuifunga Coastal Union kwenye mchezo wa ligi kuu bara licha ya mchezo wa mkondo wa kwanza, Coastal Union kufungwa mabao 3-0 na Yanga kwenye dimba la Mkapa.
Yanga inasalia kileleni ikiwa na alama 49, ikishinda michezo 14, sare 7 na kipigo 1 kwenye michezo 22, michezo mitatu mbele ya watani wake wa jadi Simba waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 45. Coastal Unioni wamepanda hadi nafasi ya kumi wakiwa na alama 26 baada ya kucheza michezo 22.
Michezo ya VPL iliyotimua vumbi jioni ya leo ni pamoja na: Mtibwa Sukari kutoka sare ya bili kufungana na Biashara United, Polisi TZ kuifunga KMC bao 1-0 huku mchezo wa watani wajadi wa jiji la Mbeya, TZ Prisons dhidi ya Mbeya City kumalizika kwa sare ya bao 1.