Rais wa Tanzania John Magufuli amefariki dunia huku akiacha kumbukumbu ya maagizo mawili ya mwisho aliyotoa wakati wa ziara yake mkoani Dar es Salaam mwezi Februari 26, mwaka huu.
Agizo la mwanzo la Rais Magufuli siku hiyo ya Ijumaa Februari 26, 2021, aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mkopo wa Sh12 bilioni uliotolewa na benki ya CRDB kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Temeke (CCM), Dorothy Kilave kuomba Serikali iwasaidie kulipa mkopo huo unaowagharimu Sh4.8 bilioni kila mwaka.
“Yaani Serikali ikalipe mkopo ambao haikuhusika, haya ni mambo ya ajabu. Mlienda kuzungumza wenyewe na benki mmeshindwa kulipa mnataka Serikali ilipe. Kuna manispaa ngapi kwa hiyo ziwe zinachukua mikopo ya wizi halafu serikali ilipe. Hilo mtalibeba wenyewe, kwanza ni kukosa nidhamu.
“Hakuna hela itakayotolewa na serikali labda kutuma wachunguzi kuchunguza kujua hizo fedha zinarudishwa kiasi gani, namuelekeza Kamanda wa Takukuru kuchunguza naona kuna ufisadi mkubwa,” alisema Rais Magufuli.
Amesema hiyo ilikuwa kawaida ya halmashauri kujiingiza kwenye ufisadi na kutumia vibaya fedha za miradi.
Agizo la pili lilihusu kuchelewa kwa malipo kwa wastaafu wa Jeshi la Polisi, ambapo Rais Magufuli alisema, “ Ni tatizo la wakubwa wenu wizarani. Niwaombe wastaafu kama mpo hapa muwalaumu Simbachawene (George) (Waziri wa Mambo ya Ndani), Katibu Mkuu na Naibu wake pamoja na wakurugenzi.
“Pia muunganishe na IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini) Simon Sirro kwa sababu hapigi kelele. Huu ndiyo ukweli wastaafu wakitaka kulipwa watalipwa, haiwezi kuchukua siku tano,” aliongeza Rais Magufuli.
Rais John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambapo alisema alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo