RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta jana Machi 12, ametangaza kurefusha kwa muda wa siku 60 marufuku ya kutoka nje usiku kama sehemu ya kukabiliana na wimbi la tatu la virusi vya corona kwenye taifa hilo.
Katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni, rais Kenyatta amesema kiwango cha maambukizo ya virusi vya corona kimepanda hadi asilimia 13 mwezi Machi kutoka asilimia 2 mwezi Januari.
Mikusanyiko ya kisiasa imepigwa marufuku kwa siku 30, marufuku ya kuwa nje usiku imerefushwa kwa siku 60 zaidi
Mabaa na kumbi za burudani kufungwa kuanzia saa tatu usiku, mazishi kufanywa chini ya muda wa saa 72, punde kifo kikitokea.
Watu wasiozidi 100 pekee ndio wataruhusiwa kuhudhuriwa mazishi na sherehe za harusi, wizara ya Afya kwa ushirikiano na ya usafiri/uchukuzi kutathmini upya kanuni za usafiri.
Kenya ambayo hadi sasa imerekodi visa 111,185 vya Covid-19 na vifo 1,899 , jana ilitangaza maambukizo mapya 829 kwa siku, idadi ambayo ni kubwa kuwahi kurekodiwa tangu mwaka uliopita.