Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema wahudumu wa afya ndio watakaokuwa wa kwanza kupokea chanjo ya Covid 19 kwani wapo mstari wa mbele katika kukabiliana na janga hilo. Kenyatta pia amewaonya wakenya kukoma kueneza uvumi kuhusu chanjo hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa chanjo ya corona katika eneo la Kitengela amesema; “…. Wahudumu wa afya walio mstari wa mbele na watoaji wa huduma ndio watakaokuwa wa kwanza kuchanjwa na sio wanasiasa’.
Tamko lake hilo linajiri baada ya kutokea ripoti kwamba wanasiasa ndio wangetangulia kuchanjwa . Uhuru amesema ni watalaam tu ndio watakaoshauri iwapo viongozi wanafaa kutangulia kuchanjwa au la.
Amesema serikali imejitolea kuhakikisha ufanisi wa shughuli nzima ya kuwachanja watu na dozi ya kwanza inatarajiwa kutolewa siku ya Ijumaa katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta. Kenya, hadi sasa watu 106,470 wamepata maambukizi ya ugonjwa huo na vifo vya watu 1,863.