Dada mwenye ushawishi mkubwa wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Kim Yo Jong ameikosoa hatua inayoendelea ya mazoezi ya kijeshi huko Korea Kusini na kuionya Marekani dhidi ya kusababisha vitendo visivyokubalika, ikiwa nchi hiyo inataka amani.
Tamko hilo limetolewa siku moja kabla ya mwanadiplomasia wa ngazi ya juu na waziri wa ulinzi wa Marekani kuwasili mjini Seoul, kwa mazungumzo yao ya kwanza kabisa na wenzao wa nchi hiyo ya Korea Kusini.
Marekani na Korea Kusini zilianza mazoezi ya kijeshi wiki iliyopita.
Kim Yo Jong ametoa ushauri kwa utawala mpya wa Marekani kwamba ni vyema isifanye hivyo ikiwa unataka amani katika kipindi chake cha miaka minne ijayo madarakani.
Hayo ndiyo matamshi ya kwanza ya moja kwa moja ya taifa hilo lenye zana za nyuklia kwa rais mpya wa Marekani, zaidi ya miezi minne tangu Rais Joe Biden alipochaguliwa kumrithi Donald Trump, japo hakumtaja Biden kwa jina.