Mungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya umetangaza kuunga mkono kikamilifu mpango wa serikali wa utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya korona.
Kwenye taarifa, Mwenyekiti wa muungano huo Askofu Philip Anyolo ameisifu serikali kwa kuweka mipango itakayohakikisha kwamba Wakenya walio hatarini zaidi wanapata chanjo hiyo.
Hata hivyo maaskofu hao wameitaka serikali kufanya kampeni ya kuwahakikishia Wakenya kuhusu ubora na usalama wa chanjo ya Oxford-AstraZeneca ili kuimarisha imani ya umma kuhusu chanjo hiyo.
“Tunaiomba Wizara ya Afya ichukue hatua zote zifaazo kuhakikishia umma kwamba chanjo hiyo ni halisi, salama na yenye ubora ili kuwatia moyo watu kukubali kuchanjwa,” akasema Anyolo.
Muungano huo pia umejitenga mbali na msimamo wa awali kutoka kwa madaktari wa katoliki ambao walisema chanjo hiyo si muhimu kwa Wakenya, na kusema kuwa hayo ni maoni yao binafsi.
“Lazima ieleweke kwamba madaktari hao hawawezi kuongea kwa niaba ya Kanisa Katoliki,” akaongeza Anyolo.
Kulingana na KCCB, Kanisa Katoliki linazingatia msimamo wa Baba Mtakatifu Francis ambaye alihimiza mataifa ulimwenguni kuhakikisha kwamba chanjo hiyo inasambazwa kote ili isaidie katika vita dhidi ya janga la COVID-19.