Maelfu ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, wakiongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021, katika hospitali ya Mzena kwa tatizo la moyo.
Shughuli ya kuaga mwili huo imeanza leo Machi 20, 2021 majira ya saa sita mchana ambapo awali mapema asubuhi, mwili wa Hayati Dk. Magufuli ulitolewa Ikulu ya Dar es Salaam na kisha kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay kwa ajili ya ibada maalum ya kumuombea.
Mara baada ya ibada kumalizika mwili wa Hayati Dkt. Magufuli, ulianza safari ya kupelekwa katika Uwanja wa Uhuru, ambapo ulipita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Morocco, Kinondoni, Mkwajuni, Magomeni, Kigogo, Ilala na Chang'ombe.
Katika maeneo yote hayo ambayo mwili wa Hayati Dkt. Magufuli, umepitishwa, wananchi wengi walijitokeza barabarani, huku wengi wakiangua vilio, kuonesha ni kwa namna gani wameguswa na kiongozi huyo aliyekuwa jemedari na mleta amendeleo kwa Watanzania wote.
Katika uwanja wa Uhuru Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwaichi, aliongoza ibada ya kuuombea mwili wa Hayati Dk. John Magufuli na kisha kufuatiwa na zoezi la kuaga mwili huo ambalo litaendelea leo na kesho kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
Mwili wa Dk. Magufuli, utaagwa Machi 22 Jijini Dodoma ambapo itakuwa ni siku ya mapumziko, kisha Machi 23 mwili wa Dk. Magufuli utaagwa katika uwanja wa Amani visiwani Zanzibar, Jumatano Machi 24 mwili wa Dk. Magufuli utaagwa Jijini Mwanza, Alhamisi Machi 25 mwili wa Dk. Magufuli utaagwa Chato mkoani Geita na mazishi ya Dk. Magufuli yatafanyika Ijumaa Machi 26 Chato, siku hiyo itakuwa ya mapumziko.