Mahakama Yavunja Ndoa Baada ya Wanandoa Kutengana Kwa Miaka 10





Mahakama ya Mwanzo Buguruni Jijini Dar es Salam leo Machi 17, 2021 imevunja  ndoa ya Magreth Silaeli (37) Mkazi wa Tabata na Raymond Kulaya (44) baada ya wawili hao kutengana kwa miaka 10 ili kila mmoja akatafute watoto  baada ya kuishi pamoja miaka mitano bila kupata watoto.

 

Awali Magreth alikuwa akiiomba Mahakama hiyo itoe hati ya talaka ili aweze kuolewa na mwanaume aliyezaa naye watoto wanne baada ya kutengana na Kulaya.

 

Akitoa hukumu hiyo leo Jumatano Machi 17, mwaka huu hakimu aliyekuwa akisikiliza Shauri Hilo, Matrona Luanda amesema wanandoa hao kwa pamoja waliieleza mahakama hiyo kuwa walifunga ndoa ya Kikristo mwaka 2006 na  hawakuwahi kuwa na watoto wala mali.

 

Hakimu Luanda amesema katika ushahidi uliotolewa na Kulaya amedai walikubaliana na Magreth kila mmoja aende anakojua ili wapate watoto.

 

Amesema baada ya kutengana kwa miaka 10, Magreth aliiomba mahakama hiyo ivunje  ndoa ili apewe talaka.

Hakimu amesema mahakama hiyo ilisikiliza shauri hilo ikielezwa kuwa mwaka 2006 walifunga ndoa na mwaka 2011 walitengana kwa makubaliano na mwanamke alipata watoto wanne  huku mwanaume akipata watoto watatu.

 

Amesema kutokana na hilo Magreth aliiomba mahakama hiyo itoe talaka kwa kuwa wametengana kwa muda mrefu.

 

Amefafanua kuwa shauri hilo lilipelekwa kwenye baraza la usuluhishi kwa sheria ya kifungu cha 101 lakini suluhu haikupatikana.

 

“Mahakama hii imepewa mamlaka ya kuvunja ndoa hii chini ya kifungu cha 107 kifungu kidogo cha 2 (f)  ya sheria ya ndoa hivyo ndani ya siku  45 asiyeridhika akakate rufaa,” amesema hakimu huyo wakati mahakama ikivunja ndoa hiyo kwa vile kila mmdaawa alikubaliana.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad