Na Paul Yohana, Geita
Ni majonzi, simanzi na huzuni ndiyo iliyotawala wilayani Chato mkoani Geita mahali ambapo Hayati Rais wa Jamuhuri ya Muungano anatokea hii ni baada ya taarifa za msiba wa kiongozi huyo ambaye alikuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumuzia msiba huu Wiliam Songoma kutoka Katoro wilayani hapa alisema kifo cha Rais Magufuli kimeacha taharuki kwa wananchi wengi wa mkoa wa Geita ambapo wamejawa na majonzi na hawajui ni nani atakuwa kimbilio lao baada yake.
"Sisi wanachato tutamkumbuka kwa maendeleo aliyoyafanya kwani alikuwa ni rais mtenda haki na alikuwa hapendi kuonea watu ni rais alitekuwa anapendeka kwa kila mtu, kwa kweli hatujui baada ya hapa," alisema
Salehe Ally mkazi wa mtaa wa Bwanga wilayani hapa alisema baada ya msiba wa Rais Magufuli wao kama wanyonge wana wasi wasi juu ya mstakabali wa maisha ya wananchi wa hali ya chini kwani kiongozi aliyefariki alipigania maslahi yao.
"Sisi wanachato tutamkumbuka kwa maendeleo aliyoyafanya, rais wetu alikuwa ni mtu mtenda haki, na alikuwa hapendi kuonea watu, na alikuwa anapendeka kwa kila mtu" alisema Salehe.
Izack Tito mkazi wa Buzirayombo wilayani hapa alisema Rais Magufuli amecha majonzi makubwa kutokana na ukweli kwamba amefanya mambo makubwa ambayo yalisifika ndani na nje ya nchi hususani katika sekta ya maendeleo ya kiuchumi.
Mwalimu wa Magufuli naye anena.
Phabian Mlingwa mkazi wa kijiji cha Buzirayombo wilayani Chato ni mwalimu wa Hayati Dk.Magufuli ngazi ya elimu ya msingi alisema kwa yeye anavyoona pengo hili haliwezi kuzibika kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao Magufuli ambao yeye ameouna tangu amufahamu.
"Mimi kama mwalimu wake niliyemfundisha shule ya msingi Chato mwaka 1972, ninasikitika sana sitopata mtumishi mwingine kama huyu aliyetuacha, tutamkumbuka kwa ujasiri na uchapakazi wake na hakuwa na upendeleo," alisema Mlingwa
Mwanafunzi wa Magufuli azungumza.
Wiliam Kabese mkazi wa mji mdogo wa Katoro wilayani Chato alisema alipokea taarifa za msiba kwa mshituko mkubwa hasa kutokana na kuwa amemufahamu Dk.Magufuli tangu akiwa mwalimu wake shule ya Sekondari Sengerema.
"Rais Magufuli kwanza amenifundish Sengerema sekondari nilimtegemea sana katika muongozo wa kulinusuru taifa hili kutoka kwenye shida na changamoto za maisha zilizokithiri kwani alikuwa kiongozi shupavu toka akiwa mwalimu wangu.
"Alikuwa ni rais wa wanyonge anasaidia kila mtu, ambaye nilimutegemea sana kulikomboa taifa letu kwani alikuwa akimusaidia kila aliyemufikia, ninashindwa kupata picha iliyoko mbele yetu," alisema Kabese.
Wachimbaji wadogo nao wamwongelea.
Kazimiri Cosmas mchimbaji mdogo wa madini katika mgodi wa msasa alisema Rais Magufuli alikuwa ni mkombozi wao ambaye watamkumbuka daima kwa kuwafanya shughuli zao zitambulike tofauti na miaka kadhaa hapo nyuma.
"Kwa sisi wachimbaji wadogo wadogo msiba wa Magufuli umetuumiza sana, hapa mgodi wa Msasa watu huwa ni wengi lakini leo wameshindwa kufanya kazi kutokana na msiba, maana kiongozi wetu aliyetuacha alikuwa ni mwadilifu, mpenda amani na mwenye upendo kwetu," alisema.
Christopher Katali alisema wachimbaji wadogo wapo kwenye majonzi makubwa kutokana na kifo cha Rais Magufuli ambaye ndiye kiongozi aliyeweka misingi rafiki kwa wao kujipatia kipato cha kila siku kupitia shughuli zao za uchimbaji.
"Zaidi alikuwa ni mtu ambaye sisi wachimbaji alitusaidia sana katika fani yetu baada ya kuingia madarakani, tuliweza kuchimba madini kwa uhuru, tunashukuru Mungu ametupatia masoko ya madini kitu ambacho kumesaidia pato la taifa kuongezeka mara dufu zaidi," alisema.
Wazee wa waliobaini karama yake ya uongozi wanamzungumuziaje
Mzee Samwel Bigambu kutoka wilayani hapa alisema alimufahamu Rais Dk.Magufuli kama kijana wake ambapo wakati linaanzishwa jimbo la Biharamulo walibaini ana uwezo mkubwa wa uongozi walimufuata na kumuomba agombee.
"Baada ya sisi kuona kwamba kuna haja ya kuwa nambubge wakati jimbo ketu linatengwa mimi na wazee wenzangu tulienda mwanza alipkuwa kampuni ya Nyanza tukaenda ofisini kwake tukamuomba agombee ubunge.
"Mwanzoni alikuwa anakana anasema mimi siyo mwanasiasa lakini kwa bahati nzuri baadaye tulizungumza naye kwa kirefu na akawa ametukubalia akaja kugombea na hatimaye 1995 akaja akawa mbunge.
Alisema miaka kadhaa baadaye wazee walipendezwa na uwezo wa Magufuli alipotumikia nyanja mbalimbali ikiwemo nafasi za uwaziri walimufuata kukushawishi kugombea urais ambapo hakuwa tayari lakini baada ya mazungumzo na ushauliano alikubali na baadaye kushinda kiti cha urais.
"Ni kijana wangu ninayemufahamu vyema sana, ni mchapakazi ambao hautokani na hamu ya uongozi bali kiu ya kutumikia watu tulimuomba akatufanyia kazi na ndiyo maana alikuwa karibu sana na wanyonge kwa sababu anafahamu shida za wanyonge,".