Makamu Wa Rais Mteule Azungumza Na Watumishi Wa Wizara Ya Fedha Na Mipango



Na Josephine Majura na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma.
Makamu wa Rais Mteule, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amekutana na Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii kutokana na umuhimu wa Wizara hiyo katika maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Philip Isdor Mpango, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango, alitoa rai hiyo jijini Dodoma alipokutana na watumishi wa Wizara hiyo katika ofisi zilizopo Treasury Square, akitokea bungeni baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge kuthibitisha uteuzi wake kwa kura za kishindo.

Dkt. Mpango amewataka watumishi wa wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuwa wizara hiyo ni moyo wa Serikali na kwamba wasipofanya kazi vizuri na kwa uaminifu hakuna miradi ya maendeleo itakayotekelezwa, mishahara haitapatikana wala mikopo itakayokopwa hivyo kukwamisha maendeleo ya wananchi.

Alisema hana shaka na uwezo wa viongozi na wataalam wa wizara ya fedha na wengine wanaoshirikiana na na kuwaomba waendeleze ushirikiano kwa viongozi wao waliobaki na Waziri wa Fedha Mpya atakaye teuliwa ili waendelee kuwatumikia watanzania, kama ambavyo walimpa ushirikiano katika kipindi chote alichofanya kazi kama Waziri wa Fedha na Mipango kwa takribani miaka 5 na nusu.

“Taifa hili ni Tajiri na kama nilivyoweka msimamo wangu huko nyuma masuala ya kuombaomba mimi sitaki na naahidi huko ninakokwenda nitalisimimia jambo hilo kwa sasabu ninaamini  kwamba Tanzania ina rasilimali nyingi, hatustahili kuombaomba na jeuri yangu ni ninyi!”. Alisisitiza Dkt. Mpango.

Aliongeza kuwa Serikali inawategemea watumishi wa Wizara kuongoza jitihada za Taifa kujitegemea kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kutanguliza maslahi ya nchi kwanza ili ndoto ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo ifikiwe.

Aliwaomba watanzania wamwombee na pia wamwombee Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuliletea Taifa hili maendeleo na kutekeleza miradi mikubwa inayoendelea pamoja na miradi mipya itakayoanzishwa lakini pia kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Aliutaka uongozi wa Wizara kusimamia vizuri makusanyo na matumizi ya Serikali ili fedha zinazopatikana ziweze kusaidia kuwaondolea wananchi umasikini kwa sababu kila mtumishi aliyepo Wizara ya fedha anabeba zaidi ya watu milioni 60 mgongoni mwake hivyo kila mtu afanye wajibu wake kwa mama Tanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwainaidi Ali Khamis, ameahidi kuendelea kushirikiana na watumishi na kumwahidi kuendeleza pale alipoachia na amemtakia majukumu mema huko aendako.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, alimshukuru Makamu wa Rais Mteule, kwa niaba ya Wizara kwa uongozi wake mahili ulioiwezesha Wizara kufanya vizuri katika kusimamia uchumi wa nchi katika kipindi chote cha miaka 5.

Makamu wa Rais Mteule Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango amehudumu kwenye nafasi hiyo kuanzia 2015 – 2021 ambapo ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anatarajiwa kuapishwa kesho (31 Machi 2021) saa 9 alasiri Ikulu- Chamwino, Dodoma

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad