Mangariba Wabuni Aina Mpya Ya Ukeketaji

AINA mpya ya ukeketaji imeibuka nchini ambao wahusika hufanya huwasugua maumbile ya siri  ya watoto wachanga kwa kutumia jiwe.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya  Wilaya ya Arusha, Angela Kiama  alisema hayo katika mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari kuhusu ukeketaji kwa wanawake na watoto, yaliyoandaliwa na asasi ya inayoshughulikia masuala ya kupinga ukatili kwa watoto ya C- Sema kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu(UNFPA).

Kiama alisema wamebaini hayo baada ya kuanza kuwakagua watoto wanaopelekwa kliniki.

“Ukeketaji mpya ulioibuka hivi sasa wanachukua jiwe lile la kusugua miguu, wanawasugua maumbile yao mpaka yanaisha, ukimkagua mtoto unakuta eneo lake la sehemu za siri jekundu sana na wanaposuguliwa wanatoka damu na inaacha makovu.

“Ndio ukatili tunaopambana nao kwa sasa, maana kila siku mangariba wanabuni njia mpya, wapo ambao wanawakeketa wakiwa wachanga tumepambana na hilo, sasa wamebuni njia hiyo nyingine ya kuwasugua kwa jiwe, tunachoomba mtu akioneka mtoto anafanyiwa ukeketaji wa namna hii aripoti haya matukio hili tuweze kufikia lengo la serikali ifikapo 2022 la kutokomeza ukeketaji nchini,”alisema.

Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) 2017/2018-2021/2022) umeeleza kwa ufasaha kwamba ukeketaji ni mila inayoathiri wanawake na watoto. Tanzania imedhamiria kukomesha kabisa ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji, kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Ofisa Uhusiano wa UNFPA, Warren Bright alisema kuelekea mwaka 2030 malengo ya Dunia, iwapo Mataifa yatasimama pamoja ipasavyo lengo namba tano katika usawa wa jinsia, UNFPA kwa kushirikiana na wadau watakuwa wametokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na mila kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana .

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa  inakadiriwa kuwa wasichana na wanawake wapatao milioni 200 wamepitia aina fulani ya ukeketaji katika nchi 30 hasa barani Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

Pia Takwimu za Kitaifa zinaonesha kuwa  mitano iliyo na kiwango cha juu cha ukeketaji ni pamoja na Manyara (asilimia 57.7 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukeketaji), Dodoma (asilimia 46.7), Arusha (asilimia 41), Mara (asilimia 32) na Singida (asilimia 30.9). Takwimu pia zinaonesha kuwa wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ambao wanaishi katika maeneo ya vijijini wana uwezekano mara mbili ya wenzao wa mijini kufanya ukeketaji (asilimia 12.7 vijijini dhidi ya asilimia 5.3 mijini).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad