WAKATI kipa wa Simba, Aishi Manula akiendelea kung’ara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumfanya Rais wa Klabu ya Al-Merrikh SC ya Sudan, Adam Sudacal kutoa ofa ya zaidi ya Sh milioni 230 ili amweze kuinasa saini ya kipa huyo, inadaiwa kuwa mabosi hao wamemfuata nchini Equatorial Guinea ili kumalizana naye.
Manula ambaye bado yupo kwenye mkataba na Klabu ya Simba anaonekana kusakwa na miamba hiyo ya Sudan, baada ya kutengeneza rekodi ya kutofungwa bao lolote Kina Lwanga wabebeshwa zigo la AS Vitakwenye mechi tatu ambazo alisimama langoni katika michezo ya Kundi A kati ya minne ambayo timu yake imecheza.
Awali mchezo wake wa kwanza katika hatua hiyo kusimama langoni ni dhidi ya AS Vita wakiwa ugenini wakashinda bao 1-0, wa pili ni dhidi ya Al Ahly ya Misri uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone.
Mchezo wa tatu dhidi ya Al-Merrikh wakiwa ugenini hakucheza kwa kuwa hakuwa fiti kiafya na nafasi yake ikachukuliwa na Beno Kakolanya, matokeo yakiwa 0-0.
Manula alisimama langoni katika mchezo wa nne dhidi ya Al-Merrikh akiokoa michomo kadhaa ambayo wapinzani walipata nafasi za wazi kwenye Uwanja wa Mkapa, Simba ikishinda kwa mabao 3-0.
Chanzo cha habari cha uhakika kimeliambia gazeti hili kuwa inaonekana harakati za Kocha Mkuu wa Al-Merrikh ya Sudan, Lee Clark anaitaka zaidi saini ya Manula ili aendelee kukiboresha kikosi hicho jambo ambalo linadaiwa kuwafanya miamba hiyo kwenda nchini Equatorial Guinea ambapo kipa huyo alikuwa akitarajiwa kusimama langoni katika majukumu ya timu ya taifa usiku wa kuamkia leo nchini humo.
“Naomba nikwambie tu kuwa ni kweli jana jioni nilisikia Manula kama anauliziwa na Waarabu flani hivi, ila kwa kuwa sikuwa na wazo lolote juu ya kutakiwa na jamaa hao kiukweli sikufatilia alichokuwa anatafutiwa.
“Isipokuwa nakumbuka nilikutana na mmoja wa wachezaji hapa, akaniambia naona dili la Aishi kwa Wasudan linaelekea ukingoni, nilipomuuliza kwa nini ndiyo akaniambia kuwa kuna jamaa kutoka Sudan wamekuja kumuona kwenye mechi yetu na Equatorial Guinea, hivyo moja kwa moja nikawa nimekumbuka,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni kulikuwa na hizo taarifa kuwa Al-Merrikh imekuwa na mpango huo wa kumuania Manula jambo ambalo muda wowote endapo Simba kupitia kwa mwekezaji wao, Mohamed Dewji ‘Mo’ watakubaliana nao juu ya ofa yao waliyotoa wakimtaka aende kujiunga na kikosi chao, inaweza kuwa dili zuri.
Lakini kwa upepo ulivyo, halitakuwa jambo jepesi kwa Simba kumruhusu mchezaji huyo kuondoka kwa kuwa wamekuwa wakiimarisha usajili wao ili kuwa bora katika ngazi ya kimataifa.