Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua madhubuti za kupambana na ugonjwa wa corona nchini, huku akiitaka kuweka wazi majibu ya vipimo vya ugonjwa huo.
Kauli ya Balozi Wright imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima kuwataka wananchi kuzingatia ushauri wa kitaalamu kupambana na ugonjwa huo.
Taarifa ya balozi huyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari juzi imesema janga la corona bado lipo na linasumbua kote duniani na kutaka hatua ziendelee kuchukuliwa.
“Ili kufahamu iwapo hatua zinazochukuliwa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa, ni muhimu sana kukusanya na kutoa taarifa na takwimu kuhusu upimaji na visa vya maambukizi.
“Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kwa serikali zote kuwasilisha kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) taarifa sahihi, na kwa wakati, kuhusu idadi ya visa katika nchi zao,” amesema Balozi Wright.
Ameendelea kusema katika taarifa hiyo kuwa kutoa taarifa hizo kunawahakikishia raia kuwa serikali zao zinapambana kulinda afya na maisha yao.
“Isitoshe, utoaji wa taarifa hizo huwawezesha watafiti na wanasayansi kufuatilia vyema zaidi ugonjwa na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika – iwe ndani ya nchi au katika kanda,” amesema.
Kuhusu chanjo, Balozi Wright ameishauri Tanzania kufikiria uwezekano wa kukubali.
“ Kama alivyosema Waziri wetu mpya wa Mambo ya Nje Tony Blinken, “Hadi pale ambapo kila mmoja duniani atakuwa amechanjwa, basi hakuna hata mmoja atakayekuwa salama kabisa.
“Chanjo zimesaidia kutokomeza baadhi ya maradhi mabaya kabisa duniani na hakuna shaka yoyote kwamba kampeni kubwa ya chanjo itaokoa maisha,” amesema.
Huku akirejea takwimu za Marekani, Balozi Wright amesema katiak wiki chache zilizopita, hasa baada ya mamilioni ya watu kupata chanjo, idadi ya wagonjwa wapya vya maambukizi ya Covid-19 imeanza kupungua.
“Ninatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukutanisha wataalamu wake wa afya na kupitia ushahidi kuhusu chanjo,” amesema.
Balozi Wright amesema nchi yake ni
mtoaji mkubwa zaidi duniani wa misaada ya kiafya na kibinaadamu na imeshatoa zaidi ya dola za Kimarekani 1.5 bilioni katika jitihada za kudhibiti COVID-19 duniani.
“Hapa Tanzania, toka kisa cha kwanza cha COVID-19 kiliporipotiwa Machi 2020, tumetoa kiasi cha dola za Kimarekani 16.4 milioni ili kukabiliana na janga hili. Marekani ipo tayari kuongeza zaidi jitihada zetu na tuna dhamira ya dhati ya kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania kuishinda Covid-19,” amesema.
Balozi Wright ambaye ni daktari wa binadamu kitaaluma aliyewahi kufanya kazi nchini miaka ya nyuma amesema ana uhakika na ushauri alioutoa.
Hata hivyo, ameipongeza Serikali kwa kutambua ugonjwa wa COVID-19 kama janga la afya ya jamii nchini Tanzania na kuwataka raia kuchukua hatua za msingi za kujilinda dhidi ya maambukizi.
Ametaja hatua hizo kuwa pamoja na kuepuka misongamano, kuvaa barakoa na kuacha nafasi inayotakiwa kati ya mtu mmoja na mwingine.