Mrema amlilia Magufuli awajia juu wanaomzushia kifo





Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Parole, Augustino Mrema amesema anaomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu John Magufuli kwa kutazama  kwenye televisheni huku akieleza maneno anayoamini ndio ya mwisho ya kuagana na kiongozi huyo.
Mrema, aliyewahi kuwa Naibu Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1993-1994) amesema Februari 2021 alizungumza na Magufuli na familia yake, mazungumzo anayoamini ni kama alikuwa akimuaga.

Mrema ni kiongozi wa kwanza wa upinzani kuteuliwa na Rais Magufuli kumsaidia kazi Julai 16, 2016 katika wadhifa wa uenyekiti wa bodi hiyo na hata muda wake ulipokwisha aliteuliwa tena.

 Mrema ambaye ni mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), alitumia nafasi hiyo kuwaonya wanaozushia kifo akisisitiza kuwa yupo hai na anaomboleza kifo cha Magufuli.

“Mimi nimeshikwa na bumbuwazi siamini sina nguvu tangu huyo bwana afariki. Yaani kwa kweli nimekuwa mnyonge kuliko maelezo. Unajua mwezi Februari wakati nakuja Salasala alinipigia simu. Ni kama vile aliniaga. Akaongea na mimi akaniuliza habari ya Parole unaendeleaje. Akaniuliza lakini hapa nina familia yangu. Kwanza nataka umsalimie dada yako anatoka kule Moshi anatoka Machame na mwingine anatoka Marangu.”

“Tukaongea kwa Kichaga pale (na wale wadada) na baadaye akaniambia msalimie mama yangu (mama Magufuli). Kwa hiyo akanipa heshima ya kumsalimia mama yake. Baadaye akaniambia nimsalimie mke wake (Janet Magufuli),” amesema Mrema.



Akizungumza kwa huzuni amesema, “ninaweza kusema Rais aliniaga ndio sababu siamini kwamba leo nimeachwa na Rais Magufuli. Hilo la kwanza nilitaka nikwambie kuwa Rais Magufuli alimuaga Mrema.”

“Kaniambia nimsalimie mama yake mzazi, nimsalimie mke wake na dada zangu wa Machame na Marangu wanaofanya kazi na yeye. Nilifiwa akaniletea Sh5 milioni kumzika ndugu yangu. Mimi ni nani nisiende kumzika yeye?”

“Hayo mambo mawili nikiyakumbuka yaani nimenyong’onyea. Yaani masikitiko yangu sina uwezo wa kufika Chato wala kuondoka hapa nyumbani. Naomboleza nyumbani niko na Tv yangu.”

Mrema amesema amempoteza rafiki mwema mwenye mapenzi  aliyemuaga, “yaani nasikitika ninaomboleza nikiwa nyumbani na mke wangu. Nalia ukiniambia hata nisimame siwezi. Ndio sababu na wengine nao wakasema nimekufa.”

OPEN IN BROWSER

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad