KIPA namba moja wa Simba na Taifa Stars, Aishi Manula akikamilisha tu dili lake la kujiunga na Klabu ya Al Merrikh ya Sudan basi kila mwezi atakuwa anakunja dola 8,000 (Sh milioni 18.4).
Takriban wiki mbili sasa timu ya Al Merrikh ya Sudan, kupitia kwa rais wao, Adam Sudacal, imekuwa kwenye nia ya wazi ya kuhitaji huduma ya Manula kiasi cha kuamua kutoa ofa ya zaidi ya 200M, hii ni baada ya kocha wa Waarabu hao, Lee Clark, kuridhishwa na utendaji kazi wake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Manula ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba, anasakwa na miamba hiyo ya Sudan kutokana na rekodi yake ya kutoruhusu bao kwenye mechi tatu kati ya nne ambazo Simba wamecheza kwenye Ligi ya Mabingwa Hatua ya Makundi.
Mchezo wa kwanza aliokaa langoni ulikuwa dhidi ya AS Vita kule DR Congo ambapo Simba walishinda bao 1-0, Mechi ya pili ilikuwa dhidi ya Waarabu wa Misri, Al Ahly pia Simba wakashinda bao 1-0 pale Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Mchezo wa tatu Manula hakucheza kutokana na kutokuwa fiti na ilikuwa dhidi ya Al Merrikh mechi iliisha suluhu lakini ile ya nne kwa Simba na ya tatu kwake alikaa angoni na Msimbazi wakaichapa Al Merrikh mabao 3-0.
Habari ambazo Championi Jumamosi imezipata kutoka chanzo cha kuaminika cha ndani ya Simba kimesema kuwa, Al Merrikh wana nia kubwa ya kumsajili Manula kwa dau la mil 230 na tayari rais wa klabu hiyo ameingilia kati kuhakikisha wanafanikisha usajili huo huku wakimuwekea mezani mshahara wa dola 8,000 (Sh mil 18.4) kwa mwezi ikiwa ni mara tatu ya ule anaolipwa Simba ambapo anakunja mil 6 kwa mwezi.
“Kadiri siku zinavyosonga mbele nazidi kugubikwa na wasiwasi juu ya uwepo wa Manula msimu ujao ndani ya timu yetu, kwani tangu taarifa za kutakiwa na Al Merreikh zilipoanza ni dhahiri kuwa jamaa wamejipanga hasa ukiangalia ofa yao na mshahara wanaotaja kumlipa.“
Ukiachia mbali dau la mil 230 la uhamisho wake, sasa ni wazi kabisa kuwa wamejipanga pia kumpatia mshahara wa zaidi ya dola efu 8, ambazo ni zaidi ya milioni 18 za Kitanzania, sasa hii inanifanya kumuona kama Mwenyekiti wa Bodi yetu, Mohamed Dewji, ‘Mo’, kama anaenda kukubali dili litiki,” kilisema chanzo hicho.
Championi Jumamosi lilimtafuta Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ili azungumzie ishu hiyo ambapo alisema: “Kwa sasa siwezi kufafanua juu ya hilo maana sipo sehemu husika ya kuelezea jambo hilo, hivyo nikuo mbe samahani sana, kwani nipo safarini naelekea msibani.
Stori: Musa Mateja, Dares Salaam