JESHI la Polisi mkoani Iringa, limemkamata mkulima wa kijiji cha Kibengu, Wilaya ya Mufindi mkoani hapa, Augustino Kiliwa (26), kwa tuhuma za kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook taarifa za uzushi za kuumwa kwa Rais Dk. John Magufuli.
Msaidizi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Rienda Millanzi, alisema mtuhumiwa huyo alichapisha taarifa hizo Machi 11, mwaka huu, kwenye ukurasa wake huo kinyume na sheria.
"Aliandika ujumbe ambao ulileta taharuki na wenye mihemko ndani ya jamii kuhusu afya ya Rais Magufuli,” alisema Malliza aliyezungumza kwa niaba ya Kamanda wa mkoa huo, Juma Bwire.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 13, mwaka huu, majira ya saa saba mchana katika kijiji cha Kibengu, kupitia kikosi maalum cha polisi kinachoshughulika na makosa ya mtandao.
Pia alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa kamanda, Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa kuwakamata wanaosambaza taarifa za uongo sio kwa Rais Magufuli, bali zozote zitakazobainika ni za uongo.
Kadhalika, jeshi hilo limewataka wananchi kujiepusha na kuchapisha ama kusambaza mitandaoni taarifa ambazo hawana mamlaka nazo kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kinyume cha kifungu namba 14 cha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni.