FIFA imeifungia madirisha mawili klabu ya soka ya AFC Leopards ya Kenya kusajili wachezaji wa kimataifa, baada kushindwa kumlipa mchezaji wao wa zamani kutoka Rwanda Vincent Habamahoro kufuatia fedha anazodai milioni 36 inayotokana na mishahara ya miezi 4.
Hili ni pigo kubwa kwa kocha mpya wa timu hiyo aliyechukua mikoba hivi karibuni, Patrick Aussems ambaye ni raia wa Ubelgiji aliyepata kuifundisha Simba Sports ya Tanzania na kufanikiwa kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi ya klabu bingwa Africa.
Aussems ambaye kwa muda mchache alioanza kuifundisha timu, ameonekana kuibadili timu hiyo mabingwa mara 13 wa ligi kuu ya nchi hiyo, licha ya kutwaa ubingwa mara hizo zote kwa mara ya mwisho ilitwaa ubingwa mwaka 1999.
Habamahoro alisainiwa na AFC Leopards mwaka 2018 akitokea nyumbani kwao Rwanda na kudumu kwa muda michache sana kufuatia timu hiyo kushindwa kumlipa mishahara ya miezi mnne mfululizo yeye na wachezaji wenzake wa kigeni Tresor Ndikumana, Ismail Diarra na Sote Kayumba.
Baada ya kuzungushana malipo hayo aliamua kuchukua hatua ya kudai maslahi yake kwa kupitia chombo cha juu cha soka yaani FIFA, baadaye chombo hicho kiliagiza mchezaji huyo alipwe na klabu hiyo kukaidi.
FIFA kwa mara nyingine imetoa siku 45 awe amelipwa kinyume na hapo ataanza kutumikia rasmi adhabu hiyo kama ilivyo kwa mchezaji wa zamani wa Yanga Amis Tambwe anayeidai klabu hiyo milioni 41.
AFC Leopards kwa sasa ipo katika nafasi ya 3 ikiwa alama 29 katika michezo 14 iliyoshuka dimbani nyuma ya alama 7 toka kwa vinara wa ligi hiyo Tusker ambayo ipo mbele michezo 2.