Gwiji wa zamani wa soka Pele amempongeza Cristiano Ronaldo baada ya mshambuliaji huyo wa Ureno kufunga mabao matatu(hat-trick)
dhidi ya Cagliari na kumfanya awe na mabao zaidi ya mchezaji nguli wa Brazil katika mechi rasmi.
Ronaldo alifunga mara tatu ndani ya dakika 32 za kwanza na kufikisha jumla 770 jumla ya mabao aliyofunga tangu alipoaanza taaluma yake - mabao matatu zaidi ya 767 yaliyofungwa na Pele.
"Maisha ni safari ya kibinafsi. Kila mmoja ana safari yake. Safari yako ni nzuri sana. Nakuenzi sana, Napenda kukutazama ukicheza na hii sio siri kila mtu anajua. Pongezi kwa kuvunja rekodi yangu ya ufungaji mabao katika mechi rasmi," Pele aliandika katika Instagram.
Baadhi ya ripoti zinaashiria mabao hayo yamevunja rekodi ya dunia lakini hilo limepingwa na Chama cha Soka cha Czech, ambacho kinadai mshambuliaji wa zamani wa Austria na Czechoslovakia Josef Bican ndiye mfungaji mabao mengi zaidi akiwa na mabao 821.
Huku hayo yakijiri, data kutoka kwa shirika la takwimu la Rec.Sport.Soccer (RSSSF) zinasema Bican alifunga mabao 805. Lakini mabao 27 kati ya hayo yalikuwa ya klabu ya Rapid Vienna na timu chipukizi ambazo hazikua mechi rasmi za kimataifa. Bican alifunga mabao 759 katika taaluma yake - nyuma ya Pele na Ronaldo.
Baada ya mechi dhidi ya Cagliari, Ronaldo alielezea kwenye Instagram kwanini sasa anatambua "rekodi" hiyo.
"Wiki chache zilizopita zilisheheni taarifa na takwimu zinazonitambua mimi kama mfungaji mabao zaidi katika historia ya soka, kupita idadi ya mabao rasmi 757 ya Pele," alisema. "Ijapokuwa nashukuru kwa utambuzi huo, sasa muda umewadia wa mimi kuelezea kwanini si kutambua hii hadi muda huu.
"Nilivyomuenzi na kuvutiwa na mister Edson Arantes do Nascimento [Pele], ndivyo ninavyoheshimu soka ya katikati ya karne ya 20 ambayo iliniwezesha kupita rekodi yake ya mabao 767, nikidhani mabao tisa ni ya timu ya taifa ya Sao Paulo, na bao moja la timu ya jeshi la Brazil, kama magoli rasmi.
Ulimwengu umebadilika tangu wakati huo na kandanda hali kadhalika, lakini haimaanishi kwamba tunaweza kufuta historia kulingana na maslahi yetu.
"Leo, nimefikia magoli 770 rasmi katika taaluma yangu, kauli yangu ya kwanza moja kwa moja inamuendea Pele. Hakuna mchezaji duniani ambaye hakulelewa akisikiliza hadithi kuhusu mchezo wake, magoli yake na malengo yake na mafanikio yake, mimi pia nilipitia hayo. Na kutokana na sababu hiyo, nina furaha na pia najivunia ninaposherehekea bao ambalo linaniweka katika orodha ya ufungaji mabao duniani, kupita rekodi ya Pele, jambo ambalo sikuwahi kufikiria wakati nilipokuwa mtoto mdogo kutoka Madeira."