LICHA ya kupoteza mchezo dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ kwa mabao 2-1, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen amewapongeza Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Iddy Nado kwa kuonyesha kiwango bora.
Mchezo huo wa kirafiki ulipigwa juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Nyayo uliopo Nairobi, Kenya.
Mabao ya Harambee Stars yalifungwa na Erick Kabailo na Abdallah Hassan huku bao pekee la Stars likifungwa na Ayoub Lyanga.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo Poulsen alisema kuwa: “Kwanza napenda kuwashukuru Harambee kwa kutuonyesha mchezo mzuri wa ushindani.“
Hii michezo ni muhimu kwetu kwa ajili ya maandalizi kuelekea michezo ya mashindano kwani tunahitaji kuona ni namna gani wachezaji wanaweza kucheza kwenye mashindano ya kimataifa.
“Tumeona kwenye eneo la ulinzi kuna makosa mengi ya kufanyia kazi ukizingatia kuna ingizo la wachezaji wapya kwenye kikosi.
“Nawapongeza Iddy Nado na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwani wamekuwa na kiwango kizuri sana kwenye mchezo huu.
“Kwa sasa tunaingia kwenye mazoezi ili kufanyia marekebisho yale makosa tuliyoyaona ili kufanya vizuri kwenye mchezo unaokuja,” alisema Poulsen.Stars inatarajia kushuka dimbani kesho kuvaana na Harambee kabla ya kuelekea Guinea kumenyana na Equitorial Guinea kwenye mchezo wa kufuzu AFCON.