Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amesema hali yake ni nzuri na anafuata ushauri wa madaktari kwa kupumzika.
Odinga alifanyiwa uchunguzi wa kawaida wa kimatibabu katika Nairobi Hospital siku ya Jumanne hatua iliyozua hofu kuhusu hali yake ya afya.
Madaktari wake wakiongozwa na daktari wake wa kibinafsi, Dk David Olunya, walisema Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa ameshauriwa kupumzika baada ya kuhisi amechoka.
"Raila alienda kufanyiwaa uchunguzi wa kawaida wa matibabu katika Hospitali ya Nairobi mnamo Machi 9 baada ya kuhisi uchovu. Amekuwa na kampeni kali na alihitaji kufanyiwa uchunguzi. Hii ilifanyika kwa mafanikio,’ amesema Dk Olunya, mtaalamu wa upasuaji wa neva.
Odinga baadaye alitumia mtandao wakijamii wa twitter kuwashukuru wote waliomtakia afuei ya haraka na akiwahakikishia kwamba hali yake ni nzuri.