Rais Mwinyi ateua mrithi wa Maalim Seif



RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, amemteua Othuman Masoud Othuman wa ACT-Wazalendo kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo, kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia 17 Februari 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu tarehe 1 Machi 2021 na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Zena Said imesema, Othuman ataapishwa kesho Jumanne, Ikulu visiwani humo.

Othuman, anachukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad (77), aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif, alifikwa na mauti wakati akiendelea na matibabu hospitalini hapo tangu 9 Februari, alipofikishwa akitokea Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.


 
Othuman, amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar.


Dk. HUssein Mwinyi, Rais wa Zanzibar
Mara baada ya Dk. Ali Mohamed Shein, kuingia madarakani mwaka 2010, alimteua Othuman kuwa mwanasheria mkuu wa serikali Novemba 2010; nafasi aliyohudumu hadi Oktoba mwaka 2014, uteuzi wako ulipotenguliwa.

Othuman alikumbana na dhahama hiyo, kutokana na misimamo yake, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Zanzibar, kwenye mchakato wa kutafuta Katiba Mpya.


Othuman, alikuwa muumini wa serikali tatu na kupigania kupunguza mambo ya muungano na kupiga kura ya wazi ya kupinga mambo kadhaa yahusiyo Zanzibar, jambo lilikuwa tofauti na msimamo wa CCM.

Kutokana na msimamo huo, Othuman alitimliwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, jijini Dodoma na kurejeshwa Zanzibar, ambako nako, alikutana na rungu la Dk. Shein la kumvua wadhifa huo.


Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo
Othuman ambaye ni mzaliwa wa Pandani, Pemba, mbali na shughuli zake za kisheria anazozifanya ndani na nje ya Zanzibar, aliendelea kusimamia msimamo wake wa haki ya Wazanzibar akiamini kwenye serikali tatu, kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif.

Ni miongoni mwa wanachama wenye kupanga mikakati ya ndani ya ACT-Wazalendo ya kuweza kuibuka mshindi na kwa kipindi chote, amekuwa karibu na viongozi wakuu wa chama hicho.


 
Othuman alianza kuwa karibu na Maalim Seif, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, na alikuwa miongoni mwa timu maalum iliyoandaa ilani ya uchaguzi huo kupitia ACT-Wazalendo.


 


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad