Wakazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamekumbwa na hofu ya kulishwa samaki wanaookotwa ziwani na wavuvi wakiwa wamekufa, baada ya kuonekana uwepo wa samaki wengi wanaoelea katika ziwa Victoria, ambao chanzo cha kifo chao bado hakijafahamika.
Wakizungumzia tatizo hilo baadhi ya wakazi hao wamesema kuwa kila mwaka kati ya mwezi Januari na Februari huonekana samaki aina ya sangara waliokufa wakielea ziwani ambao huokotwa na kutumiwa kama kitoweo, lakini wa sasa wameharibika kiasi kwamba hawawezi kuliwa, huku baadhi ya wavuvi wakidai uwepo wa samaki hao ni neema kwao.
Afisa Uvuvi mkoa wa Kagera Ephrazi Mkama, amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kutotumia samaki hao kama kitoweo, ili kuepuka kupata madhara endapo watakuwa wamekufa kutokana na kula chakula chenye sumu.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania -TAFIRI- kituo cha Nyegezi Mwanza, Enock Mlaponi, amesema kuwa wamekwishachukua sampuli za samaki hao na kuipeleka kwa Mkemia Mkuu ili kuona kama wana madhara kwa binadamu na sasa wanasubiri majibu, huku akidai kuwa inawezekana wanakufa kutokana na kukosa hewa ya oksijeni ya kutosha.