MSHAURI wa masuala ya mabadiliko wa Klabu ya Yanga, Senzo Mbatha Mazingisa, amewatuliza mashabiki wa timu hiyo na kuwaomba kuendelea kuisapoti timu yao kwani wanaendelea kupambana kujijenga ili kuwa bora zaidi.
Yanga imekuwa na mwenendo wa kusuasua katika michezo yake ya hivi karibuni ambapo Alhamisi iliyopita ilikubali kipigo cha kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Bara cha mabao 2-1 kutoka kwa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Licha ya kipigo hicho, Yanga imeendelea kushikilia usukani wa msimamo wa ligi hiyo na pointi zao 49 walizokusanya baada ya kucheza michezo 22.Akizungumza na Spoti Xtra, Senzo alisema:
“Tumepoteza dhidi ya Coastal Union, ulikuwa mchezo mgumu, ukweli ni kwamba wachezaji wetu walipambana ili kupata matokeo mazuri, lakini hali haikuwa kama ilivyokuwa matarajio yetu.“
Tunajua kuna vitu vingi ambavyo tunapaswa kuvirekebisha kama timu, tuna imani na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Cedric Kaze, tutamaliza mapungufu yaliyopo na kurejea tena katika hali ya ushindani kama ilivyokuwa awali.”