SERIKALI imetangaza kuanza kwa Tahasusi (Combination) mpya tano kwa ajili ya Wanafunzi watakaoingia Kidato cha Tano mwaka 2021 ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa Wataalamu Nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Seleman Jafo leo Machi 29, 2021 amesema Tahasusi hizo ni Fizikia, Hesabu na Kompyuta (PMC), Kiswahili, French na Chinese (KFC), Kiswahili, English na Chinese (KEC), Physical Education, Biology na Fine Art (PEBFA) na Physical Education, Geography, Economics (PEGE).
Jafo amesema Tahasusi ya PMC itatolewa katika Shule ya Sekondari ya Dodoma ambayo itakuwa maalumu kwa Wasichana ambapo kwa Wavulana itakuwa Sekondari ya Wavulana ya Iyunga.
Tahasusi ya KFC na KEC itatolewa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Morogoro na ya Wavulana Usagara wakati PEBFA na PEGE itatolewa Sekondari ya Wasichana Makambako, Sekondari ya Wavulana Kibiti na Sekondari ya Mpwapwa.
Ameomba wanafunzi waanze kuchagua kuanzia leo hadi Aprili 11, 2021 mfumo utakapofungwa saa sita usiku.