Mtu mmoja amefariki baada ya kushambuliwa na simba wawili katika hifadhi ya wanyama nchini Afrika Kusini, mamlaka zimesema siku ya Jumatatu.
Malibongwe Mfila, 27, ambaye alifanya kazi ya kufuatilia mienendo ya wanyama katika mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Marakel,amekuwa akiwatafuta wanyama katika mbuga hiyo siku ya Jumamosi aliposhambuliwa na simba hao.
Polisi wanasema alikuwa akiendesha gari kuwatafuta wanyama kama vile simba na tembo ili kutoa ushauri kwa wanaowaelekeza watalii mbugani.
Aliamua kuacha gari na kuendelea kuwatafuta wanyama kwa miguu “mara ghafla akashambuliwa na simba wawili hadi akafariki,” polisi waliongeza.
Simba hao pia waliuawa kwa kupigwa risasi.
Mwaka jana mtunzaji mashuhuri wa Afrika Kusini Mathewson Magharibu, alifariki baada ya kushambuliwa na simba alipokuwa akiwapeleka matembezi wageni katika hifadhi ya wanyama ya Limpopo.