KOCHA wa Simba Didier Gomes, Amesema kuwa timu hiyo itapambana kufa na kupona kuhakikisha kesho inaondoka na pointi tatu muhimu dhidi ya wapinzani wao Al Merrikh, katika mechi ya kundi A, Klabu Bingwa Barani Afrika.
Hayo yamebainishwa leo Machi 15, wakati kocha Gomes na nahodha wa klabu hiyo, John Bocco walipozungumza na wanahabari , jijini Dar es salaam.
“Tadeo [Lwanga] atacheza, [Pascal] Wawa ndio mchezaji ambaye atakosekana kwenye mchezo wa kesho lakini tunao wachezaji wengine wazuri ambao wanaweza kucheza nafasi yake kama Peter [Muduhwa], Kennedy [Juma] au Erasto [Nyoni] na ana uzoefu mkubwa.
“Lazima tushinde, ni muhimu sana kupata alama tatu kesho sababu kwenye hili kundi ili kufika robo fainali tunahitaji alama 11 hivyo ni muhimu sana kushinda. Kwa nilichokiona kwenye mazoezi kwa siku hizi tupo vizuri,” amesema Kocha Didier Gomes.
Naye Nahodha wa timu hiyo Bocco amesema”Tupo nyumbani na tupo tayari kupambana kwa ajili ya timu na kupata alama tatu. Tunashukuru kwa ushirikiano tunaopata kwa mashabiki ingawa tunajua kwamba kesho hawatakuwepo uwanjani lakini tunaamini kwa dua zao tutapata ushindi,” amesema Bocco.
Katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoshana nguvu kwa kutoa sare ya bila kufungana lakini katika kundi hilo ambapo kila timu imecheza mechi tatu, Simba inaongoza akiwa na pointi 7 huku Al Merreikh akivuta mkia kwa kuwa na alama moja pekee.