Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 Hababu Ally amesema wanakwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo ya vijana yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu nchini Morocco.
Akihojiwa na Kipenga ya East Africa Radio muda mchache kabla ya kupaa angani, Hababuu amesema ''Watanzania wengi wanakosea kutuhukumu kwa matokeo ya kaka zetu katika mashindano mawili yaliyopita ikiwemo CHAN iliyofanyika kule Cameroon na michuano ya vijana U-20 yanayoendelea nchini Mauritania''.
Aliongeza ''Sisi tumejiandaa vyema kwenda kupambana kwa faida ya Watanzania, tunashukuru Mwenyezi Mungu tumepata muda wa kutosha na tunaenda mapema kuzoea hali ya hewa na kucheza angalau mechi mbili kabla ya michuano ila tuombeeni sana jamani''.
Michuano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, yanatarajiwa kuanza tarehe 13/03/2021 -31/3/2021 nchini Morocco, huku Serengeti Boys wakiwahi kufika kituoni kwa ajili ya mechi kadhaa za kirafiki kabla ya zile za kimashindano.
Serengeti Boys imeondoka na msafara wa wachezaji 22 makipa 3 na wachezaji wa ndani 19 pamoja na benchi lake la ufundi, ipo katika B lenye timu za Algeria, Nigeria na Congo Brazzivile, itaanza mechi yake ya kwanza tarehe 14/03/21 dhidi ya Nigeria, kisha itarudi tarehe 17/03/21 na kumaliza mechi ya mwisho ya makundi tarehe 20/03/21 dhidi ya Congo