Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameagiza kusitishwa kwa huduma za shirika moja la ndege nchini humo baada ya ndege yake kuanguka siku ya Jumanne na kuua abiria wote.
Ndege hiyo ndogo iliokua ikiendeshwa na shirika la ndege la Supreme Sudan Kusini, ilianguka kusini mwa jimbo la Jonglei muda mfupi baada ya kuanza safari katika uwanja mdogo Pieri.
Miongoni mwa waliofariki na rubani wa Kenya, mwezake wa Sudan Kusini na abiria saba wa kike.
Katika taarifa, Rais Kiir alisema kusitishwa kwa huduma za shirika hilo ni “hatua ya muda katika juhudi za kudhibiti ajali kabla sheria za usimamizi wa safari za ndege kuimarishwa kisheria’'.