TCRA Yafafanua Malalamiko ya Simu Kitochi Kuunganishwa na Data, Bundle Kuisha Kabla ya Wakati





* Ushindani usio wenye tija wakemewa, watoa huduma watakiwa kuuza vifurushi kwa bei halisia

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) imefafanua malalamiko mbalimbali yanayotolewa na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini ikiwemo watumiaji wa simu ndogo maarufu 'kitochi' kulazimishwa kununua vifurushi vya data ambavyo hawana matumizi nayo.

Akizungumza na watumiaji na watoa wa huduma za mawasiliano, wanahabari, serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano katika semina maalumu ya kujadili kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalumu iliyotolewa kwa njia ya mtandao na Mamlaka hiyo, Mkurugenzi wa Masuala ya kisekta kutoka TCRA, Dkt. Emmanuel Manasse amesema mtoa huduma hamlazimishi mtumia huduma kununua kifurushi kinachotakiwa ni mtumia huduma kuangalia kifurushi na aina ya kifaa cha mawasiliano anachotumia.

''Mtoa huduma hamlazimishi mtumia huduma kununua vifurushi, angalia kifaa cha mawasiliano unachotumia na kifurushi unachonunua. Katika mitandao kuna vifurushi vya dakika, dakika na jumbe fupi (sms,) na vile vya dakika, sms na data ni vyema mtumiaji asome na kuchagua kifurushi kinachoendana na kifaa chake cha mawasiliano, Mamlaka ingeingilia kati hili ikiwa watoa huduma wangeweka vifurushi vya data pekee bila kujali watanzania wengine wanatumia vifaa visivyowezesha matumizi ya data.'' Amesema.

Amesema, watoa huduma wamekuwa na ushindani usio na tija kwa kuuza bidhaa za ndani za vifurushi hasa data kwa bei zisizo na uhalisia na kinachonunuliwa.

''Gharama lazima ziwe na uhalisia, tunajua watoa huduma wanajiendesha ili kupata faida na kubwa zaidi nikuwafikia watanzania wengi zaidi na kutoa huduma za mawasiliano ila bei hasa data haina uhalisia, wengi wanasema unajiunga na kupewa GB 1 ....lakini utajua utakapoipata, bando inaminywa mno hivyo TCRA imeelekeza bei za vifurushi zizingatie bei husika ya chini na juu zilizowekwa na Mamlaka.'' Amesema.

Kuhusiana na vifurushi vinavyopatikana usiku pekee Manasse amesema,

''Hilo sio kulazimishwa , watoa huduma hutoa uniti nyingi kwa wakati huo kwa kuwa hakuna watumiaji na hawawezi kuacha 'Network' bila matumizi.....wanaoweza kutumia vifurushi vya usiku wavitumie na vifurushi hivi haviwezi kutumika baada ya muda uliowekwa kuisha hata kama havijatumika.'' Amesema.

Aidha kuhusiana na malalamiko ya baadhi ya wateja kuhusiana na hoja ya kutoruhusu vifurushi vyote kuisha muda wa matumizi (Expire,)bali mtumiaji kutumia kifurushi hadi mwisho wake, Manase amesema, mteja anapojiunga na kifurushi anakubali kupewa huduma aliyonunua na kwa muda uliowekwa.

''Vifurushi hivi haviwezi kutumika baada ya muda ulioweka kuisha hata kama havijatumika na Mamlaka imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka kanuni kadhaa ikiwemo ya kumtaka mtoa huduma kuwawezesha watumiaji kuhamishiana uniti za vifurushi pamoja na mtoa huduma kumwezesha mtumiaji kununua uniti za kifurushi pindi kifurushi chake kinapokaribia kuisha ili kuokoa uniti zilizobaki ambazo zitaunganishwa katika kifurushi kipya atakachojiunga.'' Amesema.

Pia kuhusiana na malalamiko ya bando kuisha kabla ya wakati na kuminywa kwa kasi ya bando hasa kifurushi kinapokaribia kuisha Manasse amesema, simu za sauti mteja akipiga anapewa taarifa ya kiasi gani alichotumia na anaweza kulinganisha kiwango alichotumia kwa kuangalia salio na kupata ujumbe mfupi.

''TCRA imeangalia lalamiko hili na limekuja na ufumbuzi wa kuandaa mwongozo wa watumiaji kuhusiana na mfumo wa uendeshaji wa simu janja pamoja na programu Rununu zinazotumiwa na watumiaji wa data ili kulinda matumizi ya uniti zao.'' Amesema.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) imeandaa kanuni ndogo ambazo zitatua kero za watumiaji na kuongeza ustawi wa sekta ya mawasiliano na zitatumiwa kuanzia Aprili 2, 2020 ambapo watoa huduma wametakiwa kuzingatia kuwa na vifurushi visivyozidi 50 ukitoa vifurushi vya nje kwa kila mtoa huduma huku wakitakiwa kujiandaa katika utekelezaji wa kanuni hizo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad