RAIS John Magufuli alihakikisha Tanzania inaimarika katika sekta ya miundombinu ya reli kwa sababu aliamini ulimwenguni kote usafi ri wa reli ni wa gharama nafuu na pia ni kichocheo cha kukuza uchumi wa nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk Hayo aliyasema hayo jana alipozungumza na Habari Leo lilipotaka kujua maono ya Rais Magufuli kwa TRC.
Mbarouk alisema maono ya Magufuli yalisababisha ajitoe kwa moyo kuanzisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) jambo ambalo halikuwa rahisi na alifanya hivyo kwa kuthubutu kutumia fedha za Watanzania.
“Kwa hiyo mpaka sasa hivi ninavyoongea hatujaanza kuchukua fedha kutoka kwa wale ambao tunatarajia kukopa kwao, mpaka sasa tunatumia fedha za ndani, Rais Magufuli alihakikisha tunajenga reli kwa kutumia fedha zetu wenyewe kwanza na pili kama wakijitokeza watu na kufuata kile ambacho sisi tunataka, basi tunaweza kushirikiana nao ili kuimaliza reli yetu,”alisema Mbarouk.
Alisema hamu kubwa ya Rais Magufuli ilikuwa kwanza kuikamilisha awamu hii ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza.
“Alitamani hata kama muda wake utakapoisha, reli ya Dar es Salaam-Mwanza iwe imekamilika na baada ya hapo basi wengine wangeendelea kuijenga mpaka Kigoma, maana yake alitaka kuimarisha zaidi miundombinu ya sekta ya reli.”alisema Mbarouk.
Alisema Rais Magufuli alitambua kwamba usafiri wa reli hiyo ungerahisisha vitu vingi ikiwemo wafanyabiashara kupata fursa nyingi, Watanzania kujifunza vitu vingi ikiwemo teknolojia mpya na ndiyo maana aliwataka wachape kazi na wawe tayari kujifunza.
Mbarouk alisema mpaka Rais Magufuli anafariki dunia, aliacha ujenzi wa reli ya kisasa ukiendelea vizuri na kwamba, awamu ya kwanza ina vipande vitano vikiwemo vya Dar es Salaam-Morogoro, Morogoro-Makutupora, Makutupora-Tabora, TaboraIsaka na Isaka-Mwanza.
Alisema ujenzi wa kipande cha kwanza katika awamu ya kwanza cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia zaidi ya asilimia 90 na majaribio ya reli hiyo yanatarajia kuanza mwezi Agosti mwaka huu, huku ujenzi katika kipande cha Morogoro-MakutuporaSingida kikifikia zaidi ya asilimia 54.
Alisema, mpaka sasa ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea vizuri na kwa kipande cha tano cha kutoka Mwanza hadi Isaka tayari mkataba wa ujenzi umeshasainiwa tangu mwezi Desemba mwaka jana na maandalizi ya ujenzi wa kambi yameshaanza.
Katika azma yake ya kuhakikisha sekta ya reli inaimarika, Mbarouk alisema Rais Magufuli alitoa shilingi bilioni nne kwa ajili ya kukarabati mabehewa ya zamani ili Watanzania wapate huduma bora na mpaka sasa mabehewa zaidi ya 165 ukarabati wake umekamilika na fedha hizo zilikuwa zinagharamia ukarabati wa mabehewa 200.
Alisema jambo jingine ambalo Magufuli alilifanya ni kufufua njia za reli ambazo hazikutumika kwa zaidi ya miaka 30 ikiwemo njia ya Dar es Salaam-Moshi-Arusha, lakini pia alikuwa na mikakati ya kufungua njia ya Singida, Musoma na Mtwara.
“Rais Magufuli alikuwa na maono mengi na aliwekeza nguvu nyingi kwa sababu aliamini usafiri wa reli nchini ni mkombozi wa Watanzania,”alisema Mbarouk.