Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeyataka mataifa ya kigeni yenye wanajeshi na wapiganaji mamluki nchini Libya kuwaondoa haraka, huku likihimiza kusitishwa kwa mapigano baina ya pande hasimu nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa jana, Baraza la Usalama pia limetaka kuheshimiwa kwa marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya ambayo wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema imekuwa ikikiukwa.
Kupitia taarifa hiyo Baraza la Usalama pia limeikaribisha hatua iliyopigwa nchini Libya ikiwemo kura iliyopigwa na bunge la nchi hiyo siku ya Jumatano kuidhinisha serikali ya mpito iliyo na jukumu la kuandaa uchaguzi mkuu uliopangwa mwezi Desemba.
Chombo hicho kimezitaka pande zote hasimu kwenye taifa hilo lenye utajrii wa mafuta na ambalo limetumbukia vitani tangu mwaka 2011 kuhakikisha zinakabidhi madaraka kwa serikali ya mpito inayoongozwa na waziri mkuu Abdul Hamid Dbeibah.