WAKATI kipa wa Simba, Aishi Manula akiendelea kung’ara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, taarifa kutoka Sudan zinasema kwamba, Rais wa Al Merrikh, Adam Sudacal, ametoa takribani shilingi 230 kuinasa saini yake.
Waarabu hao wa Sudan, wanaonekana kuwa siriaz katika kuinasa saini ya Manula baada ya kutengeneza rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi tatu za hatua ya makundi ya michuano hiyo msimu huu.
Chanzo makini kimeliambia Spoti Xtra kuwa, Kocha Mkuu wa Al Merrikh, Lee Clark, amemuomba rais wa klabu hiyo, Adam Sudacal ampatie nafasi ya kumsajili Manula ili aendelee kukiboresha kikosi chake jambo ambalo amekubaliwa na kinachosubiriwa ni Simba kupokea ofa yake.
“Kuna uwezekano mkubwa wa Manula kutokuwa naye msimu ujao endapo Simba watakubali ofa ya Al Merrikh ambao wanamtaka kipa huyo.“Dau lao waliloweka ni dola laki moja ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 230, za Kitanzania” kilisema Chanzo hicho.
Msimu huu Manula amekuwa kwenye kiwango bora katika michuano hiyo ambapo mpaka sasa amecheza jumla ya mechi saba na kuruhusu bao moja tu dhidi ya FC Platinum hatua ya mtoano. Ana clean sheet sita. Mkataba wake unaisha 2022.