WACHIMBAJI wa mchanga wamebanwa kutokana na serikali kuweka katazo la uchimbaji bila kibali cha Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu, ambacho kitapokea ushauri kutoka kwa kikosi kazi cha mazingira.
Hayo yalibainishwa kwenye mwongozo wa usafishaji mito kwa kuondoa mchanga, taka na tope jana uliotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu kwenye kikao cha utekelezaji wa maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kuanzia leo hii (jana), shughuli zote za usafishaji mito zitakuwa zikitolewa kibali na Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu chini ya ushauri wa hicho kikosi kazi nilichokiunda hivyo basi Manispaa ndio wasimamizi wakubwa wa shughuli hizo, hivyo uchimbaji usiokuwa na kibali hautaruhusiwa na adhabu kali zichukuliwe dhidi ya wanaohusika,” alisema.
Kikosi kazi hicho kinaundwa na wajumbe kutoka Mamkala ya Bonde la Wami Ruvu, Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara (Tanroads).
Wengine ni Shirika la Reli Tanzania(TRC), maofisa mazingira wa Manispaa zote za Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) ndiye katibu wa kikosi kazi hicho.
Alisema kuwa lengo la mpango huo, siyo kuharibu kazi zilizokuwa zikifanywa na waliokuwa wakisafisha mito, ila lengo ni kuboresha kazi hizo zinufaishe badala ya kuharibu mazingira.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, mita za ujazo 6,768,000 za mchanga zilichimbwa kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
"Hii inaasharia kuwa shughuli za uchimbaji mchanga ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa madereva wa malori, wasaidizi wao, mama lishe, wabeba mchanga na wahusika wengine kwenye mnyororo wa thamani,"alisema Ummy.
Waziri Ummy alisema kuwa wizi wa mchanga, uliokuwa ukifanywa na watu hasa kwenye kingo cha madaraja kwa kisingizio cha kusafisha mto, uliishia kuharibu mazingira na kusababisha madaraja hayo kubomoka na barabara na nyumba za maeneo jirani pia kuharibika.
Alisema walichokuwa wakifanya watu hao haikuwa kusafisha mito, bali ilikuwa ni kuiba mchanga kwa kisingizio cha kusafisha mito kwa kuwa usafishaji wa mito unahusisha kuondoa taka ngumu, mchanga na matope ila wao walikuwa wakichukua mchanga.
Alisema kutokana na hali hiyo ofisi yake imeamua kuja na mwongozo huo ambao umelenga zaidi kuhakikisha mabonde ma mito yanahifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo, kuzuia mafuriko na uharibifu wa kingo za mito hatua inayosababisha mito kupanuka.
Pia imelenga kulinda miundombinu ya madaraja na nyumba za jirani ya mito husika, kuzitambua shughuli za uchimbaji wa mito na kuziratibu kama ajira rasmi kukusanya kodi stahiki zinazohusiana na uchimbaji wa michanga na zinalipwa kwenye mamlaka husika.