Waitara: Utendaji wa Magufuli ulinifanya nihamie CCM






Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na mazingira), Mwita Waitara amesema utendaji kazi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu John Magufuli ndio sababu ya kuhamia CCM akitokea Chadema ili kuunga mkono juhudi za kiongozi huyo.

Amedai utendaji huo uliua sera na hoja za upinzani na aliona ni wakati wa kujiunga na CCM kwa kuwa mengi yalitekelezwa.

Mwita aliyekuwa CCM kabla ya kujiunga Chadema alirejea kwenye chama hicho tawala Julai 2018 na baadaye CCM kilimpitisha kuwania ubunge katika jimbo la Ukonga na kuibuka mshindi.  Katika uchaguzi mkuu wa 2020,  Waitara aligombea ubunge Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM na kushinda.

Naibu waziri huyo ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 25, 2021 katika uwanja wa Magufuli  wilayani Chato kwenye  shughuli ya kumuaga kiongozi huyo.

“Huu ni miongoni mwa misiba iliyowahi kunigusa sana, aliyeniteua kwa kushirikiana na wasaidizi wake ameniamini mara mbili nikafanya naye kazi, baada ya uchaguzi akanichagua tena ni kama vile umeenda shule unasoma na kisha ukapata msiba wa anayekulipia ada lazima uumie,” amesema Waitara.

Amesema wakati msiba huo ukitangazwa alikuwa Zanzibar na ilimchukua muda kuamini kutokana na mshtuko alioupata.

Waitara amesema Magufuli alikuwa na dhamana kiutendaji na kifo chake kinawaliza wengi hasa wananchi wa kawaida.

“Mimi sikuwahi kuwa sehemu yoyote ya Serikali wala baba yangu,  yeye alikuwa mfugaji tu lakini (Magufuli) alinipa fursa. Alipoingia madarakani walisema nguvu ya soda na mimi nilikuwa mmojawao lakini rekodi yake ilitengenezwa tangu akiwa waziri rekodi ilikuwa ileile, yote aliyoyaahidi aliyatekeleza na hilo ndiyo lilinifanya nihame nilikokuwa na kuja CCM,” amesema.

Waitara alitoa wito kwa viongozi wa CCM kuhakikisha wanasimamia aliyoyafanya Magufuli kwani ndiyo ilikuwa nguvu ya wapinzani, baada ya kuyatekeleza wapinzani walikosa hoja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad