WACHEZAJI wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jemba Ulaya’ na Adolf Rishard wamesema kuwa kama klabu hiyo inataka mafanikio msimu huu, ni vema wamuache kocha wa muda wa timu hiyo, Juma Mwambusi amalize msimu akiwa anakiongoza kikosi hicho.
Hoja kubwa ya wakongwe hao ambao ni walimu wa soka kwa sasa wanadai kuwa Mwambusi anaifahamu Yanga vizuri kwa kuwa siyo mara yake ya kwanza anakaa kwenye benchi la timu hiyo, hivyo uzoefu wake utasaidia kurekebisha makosa na kurudisha makali ya timu hiyo ambayo bado ipo kileleni.
Malima alisema: “Kwanza naupongeza uongozi wa Yanga kwa kumrudisha Mwambusi kwenye benchi, kwa sababu ni kocha ambaye anaifahamu vizuri timu kwa sababu ameshakaa hapo kwa mara kadhaa, hivyo nadhani kama wangempa timu aende nayo hadi mwisho wa msimu anaweza akaipa mafanikio.
Kwa upande wa Adolf ambaye ni kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, alisema: “Ni sawa kumrudisha Mwambusi kwa sababu ni kocha ambaye ana sifa na uwezo mkubwa kwa hapa Tanzania lakini kubwa zaidi amekaa na ile timu mwanzoni mwa msimu, anawajua wachezaji wote, hivyo naona kama wangemuacha amalize msimu ingekuwa kitu bora zaidi.
”Mwambusi amerejeshwa Yanga, mara baada ya timu hiyo kutimua benchi lote la ufundi na yeye amekabidhiwa timu mpaka pale kocha mpya atakapopatikana. Mwambusi aliondoka kwenye timu hiyo kwa matatizo ya kiafya na nafasi yake ilichukuliwa na Nizar Khalfan ambaye naye ametimuliwa.