Mahakama nchini Ufaransa inatarajiwa kutangaza hukumu leo dhidi ya waziri mkuu wa zamani Edouard Balladur kuhusiana na kashfa ya miongo kadhaa ya ufadhili wa kampeni, siku chache tu baada ya rais wa zamani Nicolas Sarkozy kukutwa na hatia ya ufisadi.
Balladur mwenye umri wa miaka 91, anatuhumiwa kwa kutumia hongo katika biashara ya silaha ya miaka ya 1990 na Pakistan na Saudi Arabia ili kusaidia kufadhili jaribio lake la urais katika kesi ambayo tayari imeshuhudia watu sita wakipewa adhabu ya vifungo gerezani.
Waziri wa zamani wa ulinzi chini ya Balladur Francois Leotard, mwenye umri wa miaka 78, pia alishitakiwa. Wote wanakanusha mashitaka hayo.
Wapelelezi waligundua hongo ya kiasi cha faranga milioni 13 kutokana na biashara hiyo ya silaha, kiasi ambacho sasa ni sawa na karibu euro milioni 2.8.
Waendesha mashitaka wanataka Balladur apewe kifungo kilichoahirishwa cha mwaka mmoja jela na faini ya euro 50,000.