Waziri wa afya wa ujerumani Jens Spahn anaingia kwenye msururu wa wanasiasa wanaotajwa kuhusika na sakata la kunufaika na manunuzi ya barakoa yanyofanywa na serikali ya Ujerumani.
Ujerumani inajiandaa kuingia kwenye hatua mpya ya vikwazo vya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona kufuatia kitisho cha wimbi la tatu, huku waziri wa afya wa taifa hilo Jens Spahn akiingia kwenye msururu wa wanasiasa wanaotajwa kwenye sakata la kunufaika na manunuzi ya barakoa baada ya jina lake kujitokeza kwenye ripoti kadhaa zilizochapishwa jana Jumapili.
Makubaliano ya manunuzi ya barakoa yalifikiwa kati ya serikali kupitia wizara ya afya na kampuni ya Burda ambayo mumewe waziri huyo wa afya Jens Spahn, Daniel Funke ambaye ni mkuu wa ofisi ya kampuni hiyo mjini Berlin. Spahn anaingia kwenye orodha ya wanasiasa wa chama cha kihafidhina cha kansela Angela Merkel wanaokabiliwa na madai kama hayo.
Ripoti hiyo iliyochapishwa na gazeti la Ujerumani la Der Spiegel imesema kampuni hiyo iliiuzia wizara ya afya barakoa 570,000 zenye thamani ya dola milioni 1.08, wakati huo Spahn akiwa waziri, katika kipindi ambacho Ujerumani ilikabiliwa na wimbi la kwanza la maambukizi mwezi Aprili mwaka jana, amesema msemaji wa kampuni hiyo kufuatia ufichuzi wa mauzo hayo.
Chama cha Kansela Angela merkel kinakabiliwa na changamoto kuelekea kikao cha wakuu wa majimbo kuhusu vizuizi vya corona
Kulingana na ripoti hiyo, wizara ya afya iliilipa kampuni hiyo Euro 909,452 sawa na dola milioni 1.08. Ripoti hii ya karibuni inatolewa wakati chama cha kansela Merkel pia kikiandamwa na ukosoaji juu ya madai ya rushwa yanayohusiana na janga hilo.
Ripoti hii inachapishwa baada ya wanasiasa wawili Nikolas Loebel kutoka chama cha Merkel cha Christian Democrats, CDU na Georg Nuesslein wa Christian Social Union, CSU kujiuzulu kufuatia kashfa inayofanana na hiyo ya manunuzi ya barakoa.
Katika hatua nyingine majimbo kadhaa ya nchini Ujerumani yanaangazia kuongeza muda wa vizuizi vya kujihami na wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona hadi mwezi Aprili. Taarifa hii ni kulingana na muswada wa mkakati huo, ulioonwa na mashirika ya habari ya DPA na AFP jana Jumapili.
Mapendekezo hayo yanafuatia kuongezeka kwa visa vilivyopindukia kiwango cha juu kabisa cha maambukizi cha visa 100 kwa kila watu 100,000. Serikali awali ilitangaza kwamba hali hiyo ingetosha kabisa kupelekea kutangazwa vizuizi vipya.
Muswada huo uliangazia kiwango cha juu cha maambukizi kinachochochewa na virusi vinavyojibadilisha.
Ujerumani ilianza kulegeza vizuizi kabla ya wimbi hilo la karibuni kwa kufungua shule na baadhi ya maduka mapema mwezi huu. Kansela Merkel hii leo atakutana na mawaziri wakuu wa majimbo kuamua hatua za kusonga mbele.
Kwingineko, huko Pakistan waziri mkuu Imran Khan amepatikana na maambukizi ya virusi vya corona siku mbili baada ya kupata chanjo ya kwanza dhidi ya virusi hivyo, taarifa hii ikiwa ni kulingana na maafisa mjini Islamad.
Msaidizi wake maalumu wa masuala ya afya Faisal Sultan amesema waziri mkuu Khan amejitenga kwenye makazi yake binafsi yaliyoko Islamabad. Kulingana na serikali, chanjo hiyo ilikuwa bado haijaanza kufanya kazi kwa sababu Khan alikuwa ameipata hivi karibuni na ilikuwa ya kwanza tu kati ya mbili zinazotakikana.
Na huko China jana kuliripotiwa visa vipya saba, vikiwa vimepungua kutoka 12 vilivyoripotiwa kabla. Kulingana na tume ya afya nchini humo visa vyote vipya vilitoka nje wakati jumla ya visa vilivyorekodiwa China Bara vikifikia 90,106.