Ripoti ya pamoja ya shirika la afya duniani WHO na China kuhusu chanzo cha mlipuko wa COVID-19, inaonyesha kwamba maambukizi kutoka kwa popo kwenda kwa binadamu huenda yalipita kwa mnyama mwingine na sio kutoka maabara.
China | WHO Experten in Wuhan
Ripoti ya pamoja ya utafiti wa shirika la afya duniani WHO na China kuhusu chanzo cha mlipuko wa COVID-19, inaonyesha kwamba maambukizi ya virusi vya corona kutoka kwa popo kwenda kwa binadamu huenda yalipita kwa mnyama mwingine na sio kutoka maabara.
Utafiti huo hata hivyo umetoa mwangaza kidogo wa jinsi gani mlipuko huo ulianza na unaacha maswali mengi bila ya majibu, lakini ripoti hiyo imetoa maelezo ya kina kwanini watafiti wamefikia hitimisho hilo.
Timu ya watafiti imependekeza utafiti zaidi katika kila eneo kasoro katika nadharia ya kwamba virusi hivyo vilianzia maabara, dhana ambayo iliwahi kuelezwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuwa miongoni mwa sababu za mlipuko wa virusi vya corona.
Pia inasema kwamba dhana ya virusi hivyo kusambaa kupitia soko la vyakula vya baharini katika mji wa Wuhan China ambako kisa cha kwanza kiligundulika, haikuwa na uwezekano mkubwa. Ripoti hiyo ambayo inatarajiwa kuwekwa hadharani hii leo, inatazamwa kwa ukaribu na wanasayansi wanaojaribu kufahamu chanzo cha mlipuko wa COVID-19 ili kuweza kuzuia magonjwa ya milipuko ya baadae, lakini pia imekuwa nyeti kwa China ambayo inadai kuwa haipaswi kulaumiwa kwa mlipuko huo.
China Wuhan | Coronavirus | PK der WHO zu Untersuchungen
Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza wa Marekani Dr. Anthony Fauci amesema kwamba angependa kuisoma ripoti hiyo kabla ya kuamua juu ya uhalali wake. Mkurugenzi wa Shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ameipokea ripoti hiyo.
“Tutaisoma ripoti na kuijadili, kutathmini maudhui yake na kuchukua hata na nchi wanachama. Lakini kama nilivyosema, dhana zote ziko mezani na kunahitajika utafiti zaidi na zaidi kwa kile nilichokiona hadi sasa.”
Mwaka uliopita uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Associated Press ulibaini kwamba serikali ya China ilikuwa ikidhibiti vikali tafiti zote zinazohusiana na chanzo cha virusi hivyo. Ripoti hiyo imebainisha sababu kadhaa zinazoweza kuwa zimechangia janga hilo, lakini inaondoa uwezekano wa kwamba virusi vilianzia maabara.
Inaongeza kuwa ajali za namna hiyo huwa nadra kutokea, na kwamba maabara za mjini Wuhan zinaendeshwa vyema na hakuna rekodi ya virusi vinavyokaribiana na virusi va corona katika maabara yoyote mjini humo kabla ya Desemba mwaka 2019.
Ripoti hiyo kwa kiasi kikubwa inategemea ziara iliyofanywa na timu ya wataalamu wa kimataifa mjini Wuhan. Katika rasimu ambayo shirika la habari la Associated Press imeiona, watafiti wameorodhesha nadharia nne za uwezekano wa chanzo cha janga la virusi vya corona.
Sababu kuu inatajwa kuwa kuna uwezekano maambukizi yalitoka kwa Popo kwenda kwa binadamu kupitia mnyama mwingine. Popo wanafahamika kubeba virusi vya corona. Ripoti hiyo haijahitimisha ikiwa mlipuko huo ulianzia mjini Wuhan katika soko la vyakula vya baharini lakini soko hilo lilikuwa chanzo cha awali kwasababu ya kuuzwa wanyama wasio wa kawaida, na wengi walihoji pengine wanyama hao ndio walioleta virusi vya corona katika mji huo.